Viwanja vitano vya ndege vyenye uwezo wa kuhudumia abiria wengi

Muktasari:

  • “Tembea uone”. Ndivyo unavyoweza kusema ukifika katika viwanja vya ndege vinavyohudumia abiria wengi, hasa kutokana na ukubwa wake

Dar es Salaam. “Tembea uone”. Ndivyo unavyoweza kusema ukifika katika viwanja vya ndege vinavyohudumia abiria wengi, hasa kutokana na ukubwa wake.

Inaelezwa kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hartsfield–Jackson Atlanta (ATL) uliopo Georgia nchini Marekani ndiyo unaoongoza kwa kuhudumia abiria wengi kuliko viwanja vingine duniani.

Ndege 895,682 hutua na kuruka katika uwanja huo kwa mwaka huku ukihudumia abiria  zaidi ya milioni 107.4 kwa mwaka, sawa na wastani wa abiria 294,246 kwa siku.

Uwanja wa pili kwa kuhudumia abiria wengi ni wa kimataifa wa Beijing Capital nchini China (PEK) unaohudumia abiria milioni 100.9 kwa mwaka.

Wa tatu ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai (DXB) uliopo Falme za Kiarabu (UAE) ambao unahudumia abiria milioni 89.1 kwa mwaka hata hivyo uwanja huo unashika namba moja kwa kuhudumia abiria wa safari za nje.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Los Angeles (LAX) Marekani unashika nafasi ya nne ukihudumia abiria milioni 87.5 kwa mwaka ukifuatiwa na Tokyo International Airport (HND) wa Japani unaohudumia abiria milioni 87.1 kwa mwaka

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hong Kong (HKG) unashika nafasi ya 8 ukihudumia abiria milioni 74.5 kwa mwaka lakini ndiyo uwanja unaoongoza kwa kuwa na ndege nyingi za mizigo.

Aidha katika orodha ya viwanja 50, viwanja vya Marekani vipo vingi zaidi, katika orodha hiyo hakuna uwanja wa ndege uliopo barani Afrika.