Vyama vya CCM, Chadema ni kama fainali Kilimanjaro 2020

Muktasari:

Mara kadhaa viongozi wa CCM mkoani Kilimanjaro na wengine wa kitaifa wametoa kauli za tambo kuwa wameshapindua meza, na wamekaa mkao wa kula kuyanyakua majimbo yanayoshikiliwa na upinzani, hasa Chadema.

Mara kadhaa viongozi wa CCM mkoani Kilimanjaro na wengine wa kitaifa wametoa kauli za tambo kuwa wameshapindua meza, na wamekaa mkao wa kula kuyanyakua majimbo yanayoshikiliwa na upinzani, hasa Chadema.

Na kauli ya karibuni kabisa iliyolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akisema ameshafunga mitambo na wapinzani wasubiri kulipukiwa.

“Nikiwa Hai nilisema nina-test mitambo, sasa nawaambia tayari nimeifunga mitambo, na nimehakikisha inafanya kazi vizuri, wasubiri kulipukiwa, kwani mitambo ya kushambulia imeshasimikwa,” alisema akimaanisha chama hicho kilivyojipanga kushinda.

Lakini, ukweli ni kwamba tambo hizo zote zinatokana na nguvu ya upinzani uliopo mkoani humo.

Kabla ya Bashiru, alishakwenda Mwenyekiti wa UWT, Gaudensia Kabaka na Mwenyekiti wa umoja wa Vijana, Kheri James na kauli zao zilikuwa zilezile za kujipanga kukomboa majimbo.

 

Kilimanjaro ni moja ya mikoa ambayo ni ngome ya upinzani, likiwamo jimbo la Moshi Mjini ambalo CCM haijawahi kushinda tangu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wake wa kwanza 1995.

Kinachoikera CCM ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo iliambulia majimbo mawili kati ya tisa, sawa na ilivyokuwa mwaka 1995. Ilipata madiwani 52 kati ya madiwani 169.

Hali hiyo ndiyo inachagiza mpambano wa kisiasa na tambo kwamba katika uchaguzi ujao, CCM itanyakua majimbo yote na kuwaacha wapinzani mikono mitupu.

CCM ikisema hivyo, Chadema inaona bado iko imara katika mkoa huo, ikiamini kila mtu itakayemsimamisha katika majimbo hayo, atashinda, ikiwa uchaguzi utakua huru na wa haki.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema anasema wanaendelea kujipanga na kujiimarisha ili kujihakikishia ushindi, licha ya kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa.

“Chadema tuna uhakika, kwa maandalizi tuliyonayo tayari kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2020. Hatuna mashaka na uwezo wetu,” anasema Lema.

Lema anasisitiza maneno “uchaguzi ukiwa huru na wa haki”, kwamba hakuna muujiza wa CCM kushinda jimbo hata moja katika uchaguzi mkuu mwakani 2020 katika mkoa huo.

Anasema katika jimbo la Moshi Mjini, CCM ikipata kura 10,000 za ubunge katika uchaguzi huru na haki, lazima aombe radhi, kwa kuwa wakijipanga sana wanaweza wakaambulia kura 6,000 pekee.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumapili Julai 28, 2019