Wabunge wacharuka vitendo ya baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya

Waziri wa Tamisemi,  Selemani Jafo akijibu swali bungeni jijini Dodoma leo, alipokuwa akieleza hatua zilizochukuliwa kwa wakuu wa mikoa na wilaya wanaoweka watu ndani bila sababu za msingi na kufanya matendo yanayolalamikiwa na jamii kuwa wanashughulikiwa, licha ya kuwa kwa sasa wengi wamejirekebisha na hali imetulia. Picha na  Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Tamisemi,  Selemani Jafo amesema wakuu wa mikoa na wilaya wanaoendelea kuweka watu ndani na kufanya vitendo vinavyolalamikiwa na jamii wanashughulikiwa na kwamba si kila jambo linawekwa wazi licha ya kuwa kwa sasa wengi wamejirekebisha.

Dodoma. Baadhi ya wabunge wamelalamika kuhusu viongozi wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kufanya vitendo walivyoviita vya ovyo kwa wananchi, huku Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga akitaka wapewe tuzo wanaofanya vizuri.

Wabunge waliolalamikia vitendo vya viongozi ni Joseph Selesini (Rombo) na Mbunge Viti Maalum (Chadema) Devota Minja.

Akiuliza swali bungeni leo, Selasini amesema anatambua juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kutatua tatizo hilo.

Hata hivyo, amesema mkuu wa wilaya ya Hai amekuwa akiendelea na vitendo alivyoviita vya ovyo vya kuwakamata wawekezaji na wananchi pamoja na kushinikiza baadhi ya wanasiasa kwa kutumia askari wahame kwenye vyama vyao.

“Mkuu wa mkoa wa Iringa tulikuwa naye kwenye kikao juzi tukamwambia ajirekebishe, akatoka akaenda kutweet kuwa atakwenda kilometa 160 badala alizokuwa anaenda nazo, ”amesema.

Amesema hiyo ni  hujuma baada ya matamko yote ya mawaziri, baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya bado wanaendelea kuihujumu Serikali.

Amehoji  ni hatua gani zinachukuliwa na  Serikali kukomesha jambo hilo.

Akijibu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo amesema ni kweli awali hali ilikuwa ni  mbaya kwa sababu idadi ya waliokuwa wanafanya vitendo hivyo ilikuwa ni kubwa.

“Wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi hasa wakuu wa wilaya walikuwa wakifanya mambo yasivyo lakini tunajua sisi ndani tumefanya tathimini hali imebadilika sana,” amesema.

Jafo amesema bado kuna baadhi ya kesi wanaendelea kushughulikia na hata mambo wanayozungumza (wabunge) mengine yapo katika utaratibu wa kuyashughulikia.

“Tuvute subira si kila kitu kukitangaze public (umma)  lengo letu ni utii wa sheria bila shurti kwa wananchi wote lakini kanuni na sheria kwa viongozi wote lazima zifuatwe,” amesema.

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga amesema baadhi ya wakuu wa mikoa wanafanya kazi vizuri.

Amewataja kuwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Alli Hapi , Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander  Mnyeti, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Amehoji Serikali ina mpango gani wa kuandalia motisha ama tuzo kwa wakuu hao wanaofanya vizuri.

Akizungumzia suala hilo, Jafo amesema wakuu wa mikoa waliofanikisha ujenzi wa viwanda wamepewa vyeti hivi karibuni.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devota Minja amesema wapo makamanda wa polisi ambao hawafanyi vizuri.

Amesema yupo kamanda wa polisi anayewakataza wanaotaka kuandamana huku akitoa vitisho kuwa watakaoandamana watapigwa hadi kuchakwaza.

“Hivi kazi ya msingi kwa polisi ambao wananchi wanalipa kodi ili wapate mishahara ni kuchakaza? ”amehoji.

Akijibu, Jafo amesema jambo kubwa kuweka ushirikiano kila eneo na wananchi kufuata sheria bila shuruti ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.