Wabunge walia kupungua fedha za miradi ya maji

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imesikitishwa na kupungua kwa fedha za miradi ya maendeleo ya maji na utegemezi wa fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji katika mwaka wa fedha 2019/2020 zimepungua kwa asilimia tisa ya fedha zilizoidhinishwa mwaka 2018/19.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa amesema hayo leo Alhamisi Mei 2 wakati akisoma maoni ya kamati yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma.

Amesema tatizo la upungufu wa maji safi na salama nchini ni kubwa, ambapo upatikanaji wa maji safi ni asilimia 64.8 vijijini na asilimia 85 mjini.

Hata hivyo, amesema makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hayakidhi mahitaji makubwa ya maji kama yalivyoelezwa katika mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano ambao umebainisha maji kama kipaumbe kimojawapo cha kukuza uchumi.

“Uchambuzi uliofanywa na kamati umebaini kuwa jumla ya fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa ni pungufu kwa asilimia tisa ya fedha zilizoidhinishwa katika mwaka unaomalizika wa 2018/2020,” amesema.

Aidha, Mgimwa amesema fedha za ndani zilizoidhinishwa zimepungua kutoka asilimia 66 mwaka wa fedha 2018/2019 hadi asilimia 57 kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema utegemezi wa fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo umeongezeka kutoka asilimia 34 kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 hadi asilimia 43 kwa mwaka 2019/2020.

“Kamati imesikitishwa na kitendo cha Serikali kupunguza fedha za ndani kwenye bajeti ya maendeleo kwani  kutegemea fedha za nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa wananchi hakutoi uhakikika wa kuwapatia maji wananchi majisafi na salama kwa asilimia 95 kwa wananchi wa vijijini na asilimia 95 kwa wakazi wa mijini ifikapo mwaka 2020,” amesema.