Wabunge waliofikishwa kamati ya maadili sasa 8

Muktasari:

  • Wakati akichangia, Ruge alisema Selous ni urithi wa dunia lakini Serikali imekwenda kuharibu mazingira hayo na kuathiri maisha ya Watanzania zaidi ya 500,000 wanaofanya shughuli zao pembeni mwa Bonde la Kilombero na Mto Rufiji.

Dodoma. Catherine Ruge (Viti Maalumu-Chadema) anakuwa mbunge wanane kupelekwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma mbalimbali tangu kuzinduliwa kwa Bunge la Kumi na Moja Novemba, 2015.

Wengine ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini - ACT Wazalendo na wabunge wa Chadema, Ester Bulaya (Bunda), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele.

Jana Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alimuagiza Ruge kuwasilisha katika kamati hiyo, ushahidi kuhusu maelezo aliyoyatoa wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kuwa mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge utatekelezwa kwa Sh21 trilioni badala ya Sh6 trilioni.

Wakati akichangia, Ruge alisema Selous ni urithi wa dunia lakini Serikali imekwenda kuharibu mazingira hayo na kuathiri maisha ya Watanzania zaidi ya 500,000 wanaofanya shughuli zao pembeni mwa Bonde la Kilombero na Mto Rufiji.

Alisema kuna taarifa ya mtu anayefahamika kwa jina la George Hartiman kuwa amefanya utafiti wa tathmini ya mradi huo na kuonyesha utatekelezwa kwa Sh21 trilioni.

Alisema Serikali pia haijafanya tathmini ya mazingira ya muda mrefu. Wakati Ruge akisema hayo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliomba kutoa taarifa ya ukiukwaji wa kanuni inayotaka mbunge kutosema uongo bungeni.

Alisema mradi huo ulifanyiwa tathmini na zabuni ilipotangazwa, makandarasi waliomba, ndiyo maana wameingia nao mkataba kwa gharama ya Sh6 triloni.

“Serikali itagharamia kwa fedha zake za ndani na tayari imeshatoa asilimia 15 kiasi cha Sh685 bilioni,” alisema Mgalu.

Alisema mradi huo ambao jiwe la msingi litawekwa Julai, umeshafanyiwa tafiti nyingi ambazo hazionyeshi kama hauna faida.

Alisema pia chanzo hicho ni rahisi kwa uzalishaji, kwa kuwa umeme wa maji unazalishwa kwa Sh36, wa gesi Sh147 na wa mafuta Sh526.

Alisema megawati moja ya umeme wa joto ardhi inazalishwa kwa Sh10,039 na Sh6,000 kwa megawati moja ya umeme wa maji na kwamba Serikali imewekeza Sh32 bilioni kununua mitambo ya uchorongaji ya majaribio ya umeme wa joto ardhi.

Hata alipotakiwa na Dk Tulia kufuta maneno yake, Ruge alisema hayo ni mawazo yake na kusisitiza kwamba, mradi huo utagharimu Sh21 trilioni na hayo ameyatoa katika utafiti huo wa Hartiman na kama waziri hana, atampatia.

Akijibu kuhusu utaratibu huo, Dk Tulia alimtaka Ruge kupeleka ushahidi huo katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuangalia uhalisia wa taarifa hiyo.

Alimtaka Ruge hadi kufikia Jumatano ijayo awe amewasilisha taarifa hiyo kwa kamati hiyo.

Baada ya mwongozo huo Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema mbunge hawezi kudhaniwa kuwa amesema uongo kwa sababu amefanya rejea kutoka katika utafiti uliofanyika, jambo ambalo linaruhusiwa kikanuni.

Akimjibu, Dk Tulia alisema amemtaka mbunge huyo kwenda kwenye kamati hiyo ili wakaangalie utafiti huo pamoja na kumbukumbu rasmi za Bunge kisha kufanya uchambuzi.

Akiendelea kuchangia, Ruge alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya umeme na kama wangewekeza huko, wangepata megawati 2,100 au zaidi.

“Lakini nafahamu Wajerumani ambao hutoa fedha kwa ajili ya kuhifadhi mazingira kwenye bonde la akiba la Selou tangu mwaka 1959, wakitoa fedha kwa ajili ya kuzuia ujangili, walitoa ofa ya kuwekeza kwenye joto ardhi wakagharamia megawati 2,000,” alisema.

Akizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema wizara yake ambayo ndiyo inayohusika na mikopo, misaada na dhamana, haijawahi kupata barua rasmi yoyote kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mbadala.

“Niwaambie Watanzania, waendelee kumpuuza mheshimiwa mbunge huyu (Catherine)…Naomba nimweleze tumejiandaa, tumejipanga na tuko tayari kuutekeleza mradi huu na utakamilika kwa wakati ili Watanzania waweze kufurahia matunda yao,” alisema Dk Kijaji.

Alisema fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ipo na wala hawahitaji kwenda kuomba popote fedha.