Wachimbaji wadogo Geita watakiwa kuuza madini yao katika soko rasmi

Muktasari:

Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita waaswa kuachana na utoroshaji wa dhahabu na badala yake kutumia soko lililoanzishwa kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Mkoa wa Geita, Chrisopher Kadeo ametoa wito kwa wachimbaji wa mkoa huo kuachana na utoroshaji wa madini na badala yake kuanza kutumia soko kuu la dhahabu mkoa wa Geita.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Machi 17, 2019 wakati wa hotuba yake katika tukio la uzinduzi wa soko hilo la kwanza la madini hapa nchini.

Uzinduzi wa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa Januari 22, jijini Dar es Salaam kupitia mkutano wake na wafanyabiashara wa madini. 

“Nitoe wito kwa wachimbaji kuachana na utoroshaji madini, waanze kuuza madini yao katika soko hilo ili kulipa kodi zote za kisheria. Pia nampongeza sana Rais John Magufuli kwa kuondoa baadhi ya kodi zenye kero kwa wachimbaji wadogo nchini, chama sikivu kinazaa Serikali sikivu ambayo inaleta maendeleo kwa Watanzania,” amesema.

Soko hilo litakalofungua fursa za kiuchumi kwa mkoa huo, litahusisha wadau wote walio kwenye mnyororo wa biashara ya madini wakiwemo wanunuzi, wauzaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, benki na mamlaka ya serikali za mitaa.