Wakamatwa kwa kumuua msichana mjamzito na kumtoa kichanga chake

Muktasari:

Polisi wanasema wauaji hao walimnyonga msichana aliyekuwa mjamzito kwa waya na kumtoa tumboni mtoto mchanga, ambaye hali yake inasemekana kuwa mbaya.

 

Chicago, Marekani/AFP.Watu watatu wanashikiliwa na polisi wa Chicago kwa tuhuma za kumuua msichana aliyekuwa mjamzito, ambaye mtoto wake aliyekuwa tumboni alitolewa baada ya kufariki.

Polisi imesema Marlen Ochoa-Lopez, 19, alishawishiwa aende nyumbani kwa mtu ambaye alikuwa anamjua Aprili 23 kwa ahadi kuwa angepewa bure vifaa vitatu vya watoto, badala yake aliuawa na kichanga kutolewa tumboni mwake.

Clarisa Figueroa, 46, na binti yake Desiree, 24, wameshtakiwa kwa mauaji, wakati

Piotr Bobak, 40, ambaye polisi wamemuelezea kuwa ni mkubwa wa mpenzi wa Figueroa, ameshtakiwa kwa kuficha taarifa za mauaji.

Katika mkutano na waandishi wa habari, kamanda wa polisi wa Chicago, Eddie Johnson alielezea uhalifu huo kuwa "haukubaliki na unaotisha".

"Siwezi hata kufikiria familia inapitia katika kipindi gani kwa sasa. Walitakiwa wawe wanafurahia kuzaliwa mtoto. Badala yake wanaomboleza kifo cha mama na pengine mtoto mchanga," alisema Johnson.

Polisi wanadai waligundua mwili wa Ochoa-Lopez uliokuwa umefichwa kwenye pipa la taka wakati wakipekua nyumba ya Figueroa Jumanne.

"Ilionekana, Ochoa alinunua vifaa vya watoto kutoka kwa Clarissa, kwa hiyo walikuwa wanajuana," naibu wa kamanda huyo, Brendan Deenihan alisema.

Katika siku ambayo Ochoa-Lopez alitoweka, Figueroa anadaiwa kuzungumza naye kwa kutumia mtandao wa Facebook.

Msichana huyo mwenye umri chini ya miaka 20 aliyekuwa na mimba ya miezi tisa alikuwa akitegemea kuchukua nguo za mtoto na vitu vingine ambavyo angepewa bure.

Mamlaka zinamtuhumu Figueroa na binti yake, Desiree kuwa walimkaba msichana huyo na waya na kumtoa kitoto kichanga tumboni.

Ndani ya saa nne ambazo Ochoa-Lopez alionekana kwa mara ya mwisho kwenye kamera za usalama akiendesha gari, Figueroa mkubwa aliita huduma ya dharura akidai msichana huyo alizaa mtoto ambaye alikuwa hapumui.

Mtoto huyo alilazwa na ameripotiwa kuwa katika hali mbaya. Polisi walikataa kusema hali ya mtoto huyo kiafya.

Polisi walisema walifahamu taarifa za kupoteza kwa msichana huyo kwa mara ya kwanza kwenye mazungumzo ya Facebook na walimuhoji Figueroas Mei 7.

Walipata hati ya kupekua nyumba hiyo baada ya ushahidi wa vinasaba (DNA) kuthibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa na uhusiano na Ochoa-Lopez.  AFP