Wakili akwamisha kesi ya Halima Mdee

Muktasari:

  • Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kuendelea leo Jumanne Julai 9, 2019 katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kutokana na wakili anayeiendesha kuwa mgonjwa

Dar es salaam. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kuendelea leo Jumanne Julai 9, 2019 katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kutokana na wakili anayeiendesha kuwa mgonjwa.

Wakili wa Serikali, Glory Mwenda amedai leo mbele ya  hakimu mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini wakili, Patrick Mwita anayeiendesha ni mgonjwa.

Kufuatia maelezo hayo, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 30, 2019 na kuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi waliobaki ili kesi hiyo imalizike kwa wakati kwa kuwa ni ya muda mrefu.

Hadi sasa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi akiwemo mkuu wa kituo cha polisi cha Urafiki, mrakibu wa Polisi (SP), Batseba Kasanga.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya  Rais Magufuli kuwa,  “anaongea hovyo, anatakiwa  afungwe breki”,  kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.