Walimu watano walivyojigawa kufundisha shule yenye watoto 430

Thursday November 29 2018

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Kutokana na upungufu wa walimu unaoikabili Wilaya ya Momba umesababisha walimu watano wa Shule ya  Msingi Yala kugawana majukumu ili kuhakikisha wanafunzi 430 wanaosoma shuleni hapo wanafanya vizuri katika masomo yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi za 2017 zilizochapishwa Mei 2018, wilaya hiyo ina jumla ya wanafunzi 37,021 huku ikiwa na walimu 618.

Kulingana na idadi ya wanafunzi, wilaya hiyo  ilitakiwa kuwa na walimu 925 ili kuweza kuendana na kiwango kilichowekwa na Serikali cha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 40.

Kwa matokeo hayo na kwa mujibu wa viwango vya Serikali shule hii, inahitaji nyongeza ya walimu sita kwa sababu hivi sasa katika shule hiyo mwalimu hulazimika kufundisha wanafunzi 86 ambayo ni mara mbili ya kiwango cha serikali.

Walimu wagawana majukumu Lakini ili kuweka urahisi wa jambo hilo walimu hao walilazimika kugawana majukumu katika ufundishaji ili kila mwanafunzi apate haki yake ya kujifunza.

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Amasha Mteka anasema kutokana na darasa la awali mpaka la pili kujifunza K tatu (kusoma, kuan-dika na kuhesaabu) mwalimu mmoja analazimika kufundisha madarasa yote, huku wanne wakigawana yanayobakia.

“Tumefanya hivyo kwa sababu walimu wa madarasa ya chini huwa wana kozi maalumu ya kufundisha watoto wadogo,”

Anasema suala hilo la upungufu wa walimu limekuwa likichangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wahitimu wanaopangiwa katika eneo hilo kukimbia kituo chao cha kazi kutokana na mazingira kutokuwa rafiki.

“Kuna wengine wakifika Chitete (kijiji jirani) wakiulizwa kama wanapajua Yala wakitajiwa sifa zake wanarudia hapo,” anasema

Mmoja wa walimu katika shule hiyo Neema Kimaryo anasema, kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya walimu wamekuwa wakigawa muda ili kuhakikisha hakuna darasa linalopoteza kipindi kwa siku.

“Kwa wakati mmoja unakuwa na vipindi hadi vitano katika madarasa tofauti, hivyo unalazimika kugawa muda wa kufundisha ili kila mwanafunzi kipindi kisipite bila ya kusoma,” anasema.

Mteka anasema mbali na kufundisha wamekuwa wakijitahidi kutoa mazoezi ili kupima uelewa kuhusu walichokifundisha siku hiyo.

Mbali na walimu hao kujituma katika ufundishaji, kijiji hicho hakina huduma ya umeme huku wakazi hao wakilazimika kufuata huduma ya afya kijiji cha jirani, huku maji

yanayotumika katika eneo hilo na ukanda wote wa karibu yakionekana kuwa sio

mazuri.

Ni mwendo wa kati ya dakika 15 hadi 20 kwa pikipiki kutoka kijijini hapo hadi Chitete sehemu ambayo baadhi ya wakazi wa Yala hupata huduma za afya.

Mbali na kupata huduma hizo pia ipo Shule ya Msingi Kitete ambayo yenyewe ina walimu 15 na wanafunzi 1,060 ambayo inaonekana kuwa angalau licha ya kuwa bado mwalimu 1 analazimika kufundisha wanafunzi 70 ambao ni karibu mara mbili ya kiwango kilichowekwa na Serikali.

Lakini mwalimu Mteka anabainisha kuwa ili kupata matokeo mazuri kitaifa walimu hulazimika kuweka mkazo kwa wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani ya kitaifa ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

Hali kwingine

Lakini wakati hali ikiwa hivyo wilayani Momba katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwalimu mmoja hufundisha wanafunzi 29 kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Kwa mfano shule ya Msingi Kawe B kuna jumla ya wanafunzi 700 huku kukiwa na walimu 17. Idadi hiyo inaashiria kuwa mwalimu mmoja katika shule hiyo hufundisha wanafunzi 41 ambayo ni sawa na uwiano uliowekwa na Serikali.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli anasema idadi ya walimu waliyonayo kwa sasa inatosha kukidhi mahitaji ya wanafunzi na inawapa uhuru wa kufundisha kwa ufasaha na kueleweka.

Lakini mkurugenzi mtendaji wa Momba, Adrian Jungu anasema kutokana na mazingira ya ufanyaji kazi katika wilaya hiyo kuwa magumu kwa watumishi mbalimbali wako katika jitihada za kuboresha mazingira kwa ajili ya walimu na watumishi wengine ili wasiweze kukimbia maeneo yao ya kazi.

“Wilaya yetu bado ni mpya hivyo kila mwaka tunajitahidi kuomba kutengewa bajeti kwa ajili ya walimu wapya na watumishi wengine ili kukabilaina na upungufu uliopo sasa,” anasema Jungu.

Mbali na kuwa na mazingira magumu, Jungu anabainisha kuwa hakuna shule inayojitosheleza kwa walimu, hivyo ni ngumu kuwahamisha baadhi yao vituo vya kazi ili kuziba pengo sehemu nyingine.

Uongozi wa Mkoa

Akizungumzia hali hiyo Katibu tawala wa Mkoa wa Songwe, David Kafulila anasema ili kudhibiti wimbi la wafanyakazi kukimbia vituo vyao vya kazi na kuhamia katika maeneo yenye hali nzuri, ameamua kusitisha uhamisho kwa watumishi.

“Nimeamua kuzuia walimu kuhama kutoka Wilaya ya Momba kwenda sehemu nyingine, kwa sababu tunahitaji kuijenga wilaya hii,” anasema na kuongeza:

“Tunaamini miradi ya kimkakati iliyo mbioni kutekelezwa itaifanya wilaya hii ichangamke na watumishi wengi wapende kuishi huko.’’


Advertisement