Wana CCM 13 wajitosa kumrithi Lissu, DC Ikungi ndani

Muktasari:

  • Julai 5, 2019 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi mdogo wa ubunge wa Singida Mashariki kuwa ni Julia 31, 2019 baada ya aliyekuwa mbunge jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa za kuwa mbunge.

Ikungi. Wanachama 13 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania wamejitosa kuwania nafasi ya kupitishw ana chama hicho kuwania ubunge wa Singida Mashariki baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa.

Miongoni mwa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ni Mkuu wa wilaya  ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu na aliyewahi kuwa mkuu mkoa wa Songwe,  Chiku Galawa.

Wengine waliochukua fomu juzi na kuzirejesha jana Jumatatu Julai 8, 2019 saa 10 jioni ni Jeremia Ihonde, Lazaro Msaru, Hamisi Maulidi, Mariamu Nkumbi, Martini Lissu, Slevester Meda, Thomas Kitima, Emmanuel Hume, Mwanahamisi Mujori, Moris Mukhoty na Silinde Kasure.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya waliojitokeza kurejesha fomu,  Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Noverty Kibaji alisema wagombea hao wote kesho Jumatano watachuana kwenye mkutano wa kura za maoni.

Alisema baada ya hapo watakaoshinda nafasi tatu za juu majina yao yatapelekwa kwenye vikao vya juu vya chama na mwisho wa siku atapatikana mshindi atakayepeperushwa bendera ya CCM kuwania ubunge.

Kibaji aliwaasa wagombea hao wawe wamoja na wapendane kuanzia sasa hata baada ya mshindi kupatikana na kuwaonya kutoanzisha kampeni kabla ya muda uliowekwa

Uchaguzi huo utakaofanyika Julai 31, 2019 unatokana na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kusema Lissu kapoteza sifa za kuwa mbunge kwa kushindwa kutoa taarifa za mahali alipo pamoja na kutojaza fomu za mali na madeni.

Kutokana na hatua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ijumaa Julai 5, 2019 alitangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa ubunge utakaofanyika Julai 31, 2019.

Jaji Kaijage alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18 mwaka 2019 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 Julai 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa Julai 31, 2019.