Wanne waliokamatwa kwa tuhuma za uchochezi waachiwa

Monday January 14 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Wanaharakati wanne wakazi wa Loliondo wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, waliokuwa wanashikiliwa kwa zaidi ya siku tano kituo kikuu cha polisi Loliondo kwa tuhuma za makosa ya uchochezi hatimaye wameachiwa.

Wanaharakati hao, wakiwemo walimu wawili walikamatwa tangu Januari 8, 2019 wilayani Ngorongoro na waliachiwa jana Jumapili Januari 13 saa 12 jioni.

Wanaharakati hao, waliokamatwa ni Supuk Maoi na Clinton Kairungi walimu wa shule ya sekondari Loliondo, Kapolonto Ole Nanyoi na Manyara Karia .

Akizungumza na Mwananchi, mara baada ya kuachiwa,  Maoi alisema waliachiwa jana na leo asubuhi walitakiwa kwenda kuripoti polisi.

"Asubuhi tumeenda lakini tumeambiwa turudi  tena kesho kuripoti ila hawajatuambiwa hatma yetu" alisema.

Jana asubuhi, Januari 13, 2019, Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akitaka wanaharakati hao kuachiwa ama kufikishwa mahakamani.

Alisema kukamatwa watu hao bila kufikishwa mahakamani kwa zaidi ya siku tano ni kuvunja sheria na walitarajia kwenda mahakamani leo.

Mwangalizi wa masuala ya haki za binadamu Loliondo, Charles Ndangoya akizungumza na Mwananchi alieleza kuridhishwa na hatua ya wanaharakati hao kuachiwa.

Hata hivyo, Kamanda wa polisi Ramadhani Ng'azi  alisema alikuwa kwenye kikao hivyo angetoa taarifa baada ya kikao. "Naomba unitafute baadaye muda huu naingia kwenye kikao" alisema.

Matukio ya kukamatwa wanaharakati Loliondo yamekuwa yakitokea mara kwa mara wakituhumiwa kwa uchochezi na kutoa taarifa potofu juu ya migogoro ya ardhi Loliondo.

Advertisement