Wanywa pombe Rombo wabuni mbinu mpya ya kulewa kimya kimya

Muktasari:

  • Walevi wakiwemo wanywa gongo Rombo wamebuni mbinu mpya ya kuficha pombe kwenye koti (makoti) ili kukwepa kukamatwa na kulipa faini, huku viongozi wa dini wakiingilia kati kupinga unywaji pombe huo.

Rombo. Wanywa gongo wilayani Rombo wamebuni mbinu mpya ya kuficha pombe hizo kwenye koti (makoti) ili kukwepa kukamatwa na kulipa faini ya Sh50, 000.

Miezi  miwili iliyopita, Mkuu wa Wilaya hiyo Agness Hokororo aliagiza walevi wote wilayani humo wanaokunywa pombe hizo saa za kazi wakamatwe na kutozwa faini hiyo ili kupunguza ulevi katika wilaya hiyo.

Hata hivyo licha ya kushamiri kuendelea kwa unywaji wa pombe hizo haramu, viongozi wa jumuiya ndogo ndogo kanisa Katoliki  wameamua kuingia mtaani kukamata wanywaji na wauza gongo ili kuangalia namna ya kumaliza pombe hizo haramu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 9, 2019 Mkuu wa vikarieti ya Rombo, Padre Emmanuael Liymo ameeleza  kuwa kutokana na pombe hizo kuendelea kunyweka kama kawaida viongozi wa jumuiya wameamua kuingia mtaani kukamata pombe  hizo.

"Viongozi wetu wa Jumuiya wameamua kwenda kukamata wenyewe wauza gongo na wanywaji wa pombe hizo mtaani,” amesema  Padre  Liymo.

 Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Moru Lessoroma,  Josephat Massawe amesema kuendelea kushamiri kwa pombe hizo kunatokana na kasi ndogo ya ukamataji.

"Sasahivi vijana kwao ndio kumekucha, wanakunywa hizi pombe kama maji, kazi hawafanyi na badala yake wanaamua hata kutoa mapaa ya nyumba zao au za wazazi wao kwenda kuuza wapate hela ili wakanunua pombe,” alisema Massawe.