Washiriki maonyesho ya sabasaba waanza kupanga bidhaa

Thursday June 27 2019

Vijana wakiendelea kupanga Cd katika moja ya

Vijana wakiendelea kupanga Cd katika moja ya mabanda ya Sabasaba 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyabiashara wameanza kupanga na kusogeza mizigo yao katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo Maonyesho ya Biashara ya 43 ya Kimataifa Sabasaba  yatakapofanyika.

Maonyesho hayo yatakayoanza kesho Ijumaa Juni 28 hadi Julai 13, 2019 yanatarajia kushirikisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 35.

Leo Alhamisi Juni 27, 2019 Mwananchi limefika katika viwanja hivyo na kushuhudia maandalizi yakiendelea kwa washiriki kupanga vitu mbalimbali huku mabanda mengine yakionekana kuwa wazi.

Mmoja wa wafanyakazi waliokutwa wakishusha majokofu katika gari amesema leo ndiyo siku ya mwisho kusogeza vifaa hivyo huku kesho akiitaja kuwa siku ya kuanza kutoa huduma.

“Vitu vyetu vinahitaji ubaridi hivyo ni lazima tuanze kuleta hivi kwanza kabla ya bidhaa na leo ndiyo siku ya mwisho kufanya maandalizi kesho ni kuruhusu tu wananchi watembelee mabanda yetu wapate huduma,” amesema mfanyakazi huyo bila kutaka jina la kampuni wala lake.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya African Creative inayohusika na kuweka vitabu vya masomo mbalimbali katika CD, Renatus Siantemi amesema atatumia maonyesho hayo kuonyesha umuhimu wa kutumia CD  kuhifadhi vitabu.

Advertisement

“Napenda kesho nianze kazi rasmi siyo nianze kuhangaika kupanga, sidhani kama itafanyika vile, ndiyo maana nimeamua kuwahi ili nikamilishe kila kitu mapema” amesema Siantemi

Advertisement