Watanzania wawili wakamatwa Kenya kwa biashara ya dhahabu feki

Baadhi ya Watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka likiwemo la kijihusisha na biashara ya kuuza dhahabu feki nchini Kenya wakiwa kizimbani baada ya kufikishwa na kusomewa mashtaka katika Mahakama iliyopo Kaputei Gardens, kilimani nchini humo juzi. Picha na Dennis Onsongo

Muktasari:

  • Inaelezwa kuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliagiza kufanyike msako baada ya kupata malalamiko ya wafanyabiashara hao haramu kumtapeli mwana wa mfalme wa nchi ya Falme za Kiarabu.

Dar es Salaam. Watanzania wawili ni miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa hivi karibuni wakidaiwa kujihusisha na biashara haramu ya dhahabu feki nchini Kenya kutokana na msako mkali unaofanywa nchini humo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Star wa Kenya, Watanzania hao ni pamoja na Manson Mtassi na Konie Kalist. Wengine waliokamatwa ni pamoja na Chikunosho Francis Ogbuanu wa Nigeria na Ruhota Kabagale wa Congo.

Mbali na raia wa kigeni, raia wa Kenya pia hawakukosekana, tovuti ya Standard Digital ya nchini humo imewataja kuwa ni pamoja na Boniface Mtwasi, Robert Riagah, Caleb Otieno na Michael Omondi.

Washukiwa hao walikamatwa mwezi uliopita na askari kanzu eneo la Kiboko barabara ya Mukoma wakiwa na mamilioni ya dola na dhahabu feki.

Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Siro alipoulizwa na Mwananchi jana kama ana taarifa za kukamatwa kwa Watanzania hao alisema jeshi hilo halina taarifa.

Inaelezwa kuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliagiza kufanyike msako baada ya kupata malalamiko ya wafanyabiashara hao haramu kumtapeli mwana wa mfalme wa nchi ya Falme za Kiarabu.

Mbali na watuhumiwa hao, mtandao huo wa Star pia umeandika kuwa Jumatatu iliyopita kikosi cha askari kanzu cha Kenya kilivamia nyumba moja eneo la Kileleshwa jijini Nairobi na kukamata dhahabu feki na magari manane na washukiwa wanane.

Pia, vitu mbalimbali vilikamatwa katika nyumba hiyo iliyokuwa ikilindwa na maofisa wa usalama.

DCI wa Kenya, George Kinoti alisema katika ujumbe wake wa Twitter kuwa magari yaliyokamatwa na dhahabu feki yalikuwa yakitumika kutapeli wananchi.

Wiki iliyopita, mmoja wa wafanyabiashara aliyedaiwa kutaka kumtapeli mwana wa Mfalme wa Dubai kwa kumuuzia dhahabu feki alikamatwa na polisi katika duka la Lavington.

Hivi karibuni, DCI Kinoti alizishauri balozi zote nchini humo kuwatahadharisha wananchi wao kuhusu jambo hilo.

Aliandika “utapeli wa dhahabu sasa umefikia pabaya, baadhi ya wageni wa mataifa mengine wamekuwa wakitapeliwa na kutoa fedha nyingi kwa matapeli.

“Tahadhari hii ya DCI imetolewa ili kuzuia uhalifu kutokana na kesi zinazohusisha ununuzi na uuzaji wa dhahabu nchini.”