Watatu mbaroni mauaji kiongozi wa Chadema

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbroad Mutafugwa

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu watatu kwa kutuma za mauaji ya Katibu mwenezi wa Chadema wilaya ya Malinyi.

Morogoro.  Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya katibu mwenezi wa Chadema Wilaya ya Malinyi, Lucas Lihambalimu (42).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Juni 14, 2019 Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbroad Mutafugwa amesema tukio hilo la mauaji limetokea  Juni 13, 2019  saa 8 usiku katika kijiji cha Munga tarafa ya Mtimbira wilayani Malinyi.

Amesema uchunguzi uliofanywa imebainika chanzo cha mauaji ni  mgogoro wa mashamba.

Mutafungwa amesema kada huyo alikuwa na wake wawili  Anastazia Sandi (42) na Zaituni Matandiko (42).

Amesema siku ya tukio katibu huyo alikuwa amelala na mkewe mdogo,  alisikia vishindo vya watu wakitembea nje ya nyumba yao.

“Alimwamsha mkewe na kumwambia kuwa kuna watu wapo nje ya nyumba, alichungulia kupitia uwazi uliopo kati ya paa na ukuta, na alifanikiwa kuwaona watu watatu na kumtambua mmoja."

 “Aliwaona hao watu wakielekea upande mwingine wa nyumba yao na  alienda kuchungulia tena ndipo aliposikia mlipuko wa bunduki na kumueleza mkewe kuwa wamempiga na kurudi kitandani akiwa anavuja damu kichwani,” amesema.

Amesema shambulio hilo wananchi walienda kutoa taarifa kituo cha polisi, askari walifika eneo la tukio na kukuta kipande kidogo cha chuma chenye umbo la duara kinachotumika katika bunduki zilizotengenezwa kienyeji.

Amesema walianza msako kutokana na tukio hilo polisi kwa kushirikiana na wananchi na kuwakamata watu watatu.

Mutafungwa amesema mwili wa katibu huyo ulifanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika jana Alhamisi  Juni 13, 2019.