VIDEO: Watoto 3 waliochinjwa ni wa familia moja

Muktasari:

Katika jitihada za kudhibiti mauaji hayo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri alise-ma wameanza na kusajili watu wote mitaani katika vitabu maalumu.

Njombe/Dar. Watoto watatu kati ya 10 waliotekwa na kukutwa wakiwa wamechinjwa wilayani Njombe ni wa familia moja.

Watoto hao; Godliva Mwenda (11), Gasper Nziku (8) na Giliad Nziku (5) wote wa Danford Nziku walichukuliwa na mtu ambaye hajafahamika walipokuwa wakicheza nyumbani kwao katika Kijiji cha Ikando, Kata ya Kichiwa ambako walichinjwa kisha kunyofolewa viungo vya mwilini.

Walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ikando. Godliva alikuwa darasa la nne, Gasper la kwanza na Giliad alikuwa darasa la awali.

Walivyotekwa

Charles Mlonganile, akisoma historia ya marehemu hao kwa niaba ya familia ya Nziku katika mazishi yao yaliyofanyika jana, alisema watoto hao walichukuliwa na mtu nyumbani kwao saa moja jioni Januari 20. Alisema wakati wakichukuliwa, walikuwa watano wote wakicheza nje ya nyumba yao.

“Walibaki watoto wawili hapa nyumbani na walipoulizwa wenzao wako wapi, walisema wamechukuliwa na Joely Nziku,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Rashid Ngonyani alisema wanamshikilia Joely, mkazi wa Makambako ambaye ni ndugu wa baba wa watoto hao kwa mahojiano.

Alisema baada ya hapo jitihada za kuwatafuta zilianza kwa ndugu, wananchi na Serikali kupitia Polisi na juzi walipata taarifa kwamba kuna watoto wamepatikana wakiwa wamefariki na ndugu walipokwenda polisi waliwatambua.

Naibu waziri ahudhuria mazishi

Akizungumza katika mazishi ya watoto hao, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema wote waliohusika na tukio watasakwa na kutiwa nguvuni.

“Poleni sana ndugu zangu, niwahakikishie Watanzania na ndugu wa familia hii kwamba tukio hili halitapita burebure. Tunataka iwe fundisho kwa watu wengine wote wenye roho za kinyama na kishenzi waliotekeleza mauaji haya,” alisema.

Alisema baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa na vyombo vya dola vinaendelea kudhibiti na kushughulika na mtandao wa wauaji hao wa raia wasiokuwa na hatia wakiwamo watoto.

Wataka mbinu za Kibiti

Baadhi ya wazazi waliozungumzia tukio hilo jana waliiomba Serikali kushughulikia matukio hayo kama ilivyofanya katika mauaji ya Kibiti, Pwani.

Mkazi wa Njombe, Yunus Mfugale alisema, “Mbinu zilizotumika Kibiti tunaomba zitumike katika jambo hili. Inatisha unaweza kuona jambo kama dogo lakini wenye watoto wanapata taharuki. Kuna mbinu za msingi zilizotumika Kibiti zitumike Njombe.”

Mkazi wa Mtwango, Njombe, Atuganile Kilasi alisema, “Hofu imetanda na mauaji yametokea siku nyingi, polisi waongezewe nguvu hawa wauaji inaonyesha wamejichimbia kwenye misitu.”

Mbali ya kuzua taharuki, Joseph Mbwilo mkazi wa Njombe alisema mauaji hayo yanaweza kuwa chanzo cha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi iwapo hayatadhibitiwa kwa wakati.

“Watoto wanaishi kwenye hofu na hata ufaulu Njombe huenda ukashuka kwa maana wanakaa shuleni kwa wasiwasi, imefikia hatua hata mtu akimkaribia mtoto akanyanyua mkono mtoto anaogopa anahisi anakamatwa.”