Watoto 10 wachinjwa Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka

Muktasari:

  • Matukio ya watoto wa umri kati ya miaka miwili hadi sita kuchinjwa na kukatwa koromeo, sehemu za siri na ulimi wilayani Njombe yanahusishwa na imani za ushirikina, visasi na tayari vyombo vya ulinzi vimeagizwa kupitia upya leseni za waganga wa jadi na kuwakamata wanaohusishwa na vifo vya watoto hao.

Dar es Salaam. Watoto 10 wenye umri kati ya miaka miwili hadi sita wamechinjwa na kukatwa koromeo, sehemu za siri, masikio na ulimi wilayani Njombe mwezi huu.

Kutokana na matukio hayo yanayodaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina, mkuu wa wilaya hiyo, Ruth Msafiri ametoa amri kwa wazazi na walezi kuwapeleka na kuwafuata shule watoto wao. Pia, ameagiza watoto wote wilayani humo kuhakikisha kuwa wanatembelea kwa makundi.

Aidha, mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema, “Imani za ushirikina na malipizo ya visasi ndivyo vinaleta haya mambo, nimeagiza vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi kupitia upya leseni za waganga wote wa jadi na kuwakamata wale wote wanaohusishwa kutoa maelekezo yanayosababisha vifo vya watoto na watu wazima kwa imani za kishirikina.”

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema taarifa alizonazo ni za matukio mawili ambayo polisi wanayafanyia kazi.

Lakini wakati Lugola akisema hayo, Msafiri alisema mtoto wa 10 aliokotwa jana akiwa amechinjwa na kunyofolewa viungo. Alisema watoto sita wamefanyiwa ukatili huo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na wanne wanatoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

“(Kati ya) sita waliookotwa (wakiwa wamekufa) Halmashauri ya mji Njombe, wawili walipotea na kuokotwa wakiwa wameuawa misituni, wawili wameokotwa maeneo tofauti wakiwa wamekufa na hawakutambulika, wamezikwa na halmashauri,” alisema.

Alisema mmoja alikatwa koromeo na aliokotwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, “Mtoto mmoja ameokotwa leo (jana – akiwa amekufa) Mto Hagafilo.”

Alisema kati ya hao wanne waliookotwa katika Halmashauri ya Wilaya Njombe, watatu walitekwa na hawajapatikana mpaka sasa.

Msafiri alisema kutokana na hali hiyo, jana alikutana na viongozi wa madhehebu ya dini, mitaa, madiwani na kamati yake ya ulinzi na usalama na kuanzisha ulinzi mitaani.

“Tunatoa pia mafundisho na kupiga vita waganga wa kienyeji, ramli chonganishi na vyombo vyote vya usalama viko kazini kwa bidii yote,” alisema.

Mkazi wa Chaugingi, Atupele Sanga alisema tangu shule zilipofunguliwa wiki tatu zilizopita, amekuwa akiwapeleka na kuwafuata watoto shule.

Mkazi wa Njombe Mjini, Nicholaus Mhando alisema utekaji huo unatisha kwani wapo wazazi watatu waliopokonywa watoto na watu wasiojulikana na baadaye wakawakuta wameuawa.

Mmoja wa walimu wa shule ya msingi mjini Njombe ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, “Ninafundisha darasa la kwanza, kulingana na umri wao inaniwia vigumu kuwaruhusu kuondoka, kila mtoto anachukuliwa na mzazi wake. Siwezi kukubali hali hii imkute mwanafunzi wangu. Wapo wanakaa mpaka muda mbaya ila mpaka mzazi aje nami ndiyo narudi nyumbani,” alisema.

Akizungumzia matukio hayo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema, “Hili lina sura nyingi. Ni jinai, wenzetu wa ulinzi na usalama wanalishughulikia sisi Wizara ya Afya limetugusa katika masuala ya maendeleo ya mtoto na tiba asili.”

Alisema kupitia Serikali ya mkoa imeitisha mkutano wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuzungumzia suala hilo.