Watoto wawili marafiki wajinyonga

Muktasari:

  • Ofisa mtendaji wa kata ya Magugu, Daniel Limbu alisema vifo hivyo vya watoto kujinyonga vimesababisha mshangao mkubwa kwa jamii katika eneo hilo.

Dar es Salaam. Kifo cha mtoto, Jasmine Ngole aliyejiua kwa kujipiga risasi hivi karibuni kinaendelea kusumbua akili za wazazi na walezi nchini.

Wakati kabla tukio hilo halijapoa, tukio jingine la watoto wawili kujiua kwa kujinyonga limetokea mkoani Manyara.

Katika tukio lisilo la kawaida, watoto wawili wa darasa la tano waliokuwa wakikaa dawati moja katika Shule ya Msingi Mikiroy wilayani Babati mkoani Manyara wamefariki dunia kwa kujinyonga katika matukio mawili tofauti.

Akizungumzia matukio hayo mjini hapa jana, kamanda wa polisi mkoa huo, Augostino Senga alisema la kwanza lilitokea juzi saa 11:00 jioni kwenye kata ya Magugu.

Alisema katika tukio hilo mtoto Mathayo Ezekiel (11) aliporudi nyumbani kwao jioni kutoka shule aliwakosa wazazi wake na kufuata funguo zilizokuwa zimehifadhiwa kwa jirani na baada ya kufungua mlango aliingia ndani na kujifungia chumbani ambapo alijinyonga kwa kutumia taulo hadi akapoteza maisha.

Alisema tukio la pili, mwanzoni mwanafunzi mwenzake alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kanga.

Alisema mwanafunzi huyo Hamis Juma (11) ambaye alikuwa anasoma darasa la tano kwenye shule hiyo hiyo alifariki dunia kwa kujinyonga akiwa nyumbani kwao Magugu.

Ofisa mtendaji wa kata ya Magugu, Daniel Limbu alisema vifo hivyo vya watoto kujinyonga vimesababisha mshangao mkubwa kwa jamii katika eneo hilo.

Alisema Ezekiel alikuwa akiishi na mama yake na baba wa kambo baada ya mama yake kutengana na baba yake mzazi.

Aliwataka wazazi na walezi kuwa waangalifu wakati wa makuzi kwani wanapaswa kuwa karibu na watoto wao na kujua kila hatua ya maisha yao na mambo wanayokumbana nayo na kuwataka kwa pamoja kuwapa upendo wa wazazi ili wajisikie wapo salama.

Tukio hilo ni wazi linaibua hali ya wasiwasi kwa wazazi na walezi hasa wanapolihusisha na tukio la Jasmine ambaye alijiua kwa kujipiga risasi mkoani Morogoro.

Jasmine alijiua akitumia bastola mali ya Profesa Hamis Maige.

Rafiki wa Jasmine, Imelda Mlanzi ambaye alizimia wakati wa mazishi wa Jasmine alisema kwamba aliachiwa shajara na marehemu saa chache kabla hajaamua kujiua na kuambatanisha fedha taslimu Sh 20,000.

“Aliniambia katika hizi Sh 20,000, Sh 10,000 nichukue na zilizobaki nilipe madeni kwa watu wanaomdai,’’ alisema Imelda ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lupanga.

Mbali na hilo katika shajara hiyo pia Jasmine alijielezea kuwa yeye ni mtoto asiyewajua wazazi wake na asiyejua kazaliwa wapi. “Mtoto huyu anatamani kukiona kifo chake wakati wowote, mtu yeyote atakayesoma diary (shajara) hii ndiye atakayeandika siku ya kifo.

Muda mfupi baada ya kutokea tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbrod alisema kwamba mmiliki wa bastola hiyo, Profesa Maige alijitokeza na kueleza kuwa ndiye mmiliki halali wa bastola hiyo.

Kwa upande wa Imelda alisema Jasmine alikuwa na tabia ya kuzungumzia kifo chake akisema kinakaribia na kwamba kitakuwa kibaya kiasi cha watu kushindwa kuuaga mwili wake.

“Hakuwahi kueleza hali ya maisha anayaoishia nyumbani kwao na hata nilipokuwa nakwenda kwao nilikuta akiishi katika maisha mazuri na hata mahitaji ya shule alikuwa akiyapata kama kawaida yeye na mdogo wake ambao walikuwa wakipelekwa shule kwa gari dogo la nyumbani.