Waziri Mkuu Tanzania abaini kasoro Uwanda wa Ndege, atoa maagizo

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa maagizo kadhaa kwa viongozi wa Serikali nchini humo hasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhakikisha yanafanyiwa kazi haraka kabla ya kuanza kwa shughuli za Mkutano 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Dar es Salaam

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Taznania, Kassim Majaliwa amekagua jengo la tatu la abiria kwenye kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere ili kuona maandalizi ya mapokezi kwa wajumbe wa mkutano wa wa 39 wa Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). 

Mikutano hiyo itakaofanyika Agosti 5 hadi 18, 2019 ikiwemo Mkutano Mkuu wa Wakuu wa nchi za SADC utafanyika Agosti 17 na 18 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Akizungumza na watendaji wa Serikali pamoja na Kamati ya maandalizi uwanjani hapo leo jioni Jumatano, Julai 31, 2019, Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa amesema maandalizi ni mazuri isipokuwa kuna kasoro chache zilizobakia.

“Nimepita VIP hakuna shida. Pale terminal 2, sehemu ya uhamiaji iko vizuri, uchunguzi wa afya nayo iko vizuri, lakini vyoo inabidi vibadilishwe haraka sana. Vile vyoo pale nje vimechoka, vibadilishwe mara moja, siyo tu kwa ajili ya ugeni, bali ni kwa faida yetu pia,” amesema Majaliwa huku akimwagiza meneja wa uwanja huo, Paul Lugasha aharakishe shughuli hiyo 

Katika jengo la tatu la abiria kwenye uwanja huo, Waziri Mkuu huyo wa Tanzania amekagua eneo ambalo viongozi wakuu wa nchi watashukia, watakagua gwaride la heshima na kuangalia vikundi vya ngoma. Pia amekagua vyumba ambavyo watapumzikia kabla ya kuelekea mjini.

Majaliwa amesisitiza kuwa usafi wa barabarani bado hauridhishi sababu kuna mawe, udongo na michanga kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege hadi mjini.

“Tulikubaliana kuwa zile bustani ziboreshwe, vyuma vya barabarani vitengenezwe lakini hata leo nimepita kwenye fly-over, bado kuna mawe na michanga, hata sijui vinatokea wapi,” amesema Majaliwa 

Amewataka wahusika waweke banners za kutosha za aina mbalimbali na picha za wanyama kutani, uwanjani hapo ili kuonesha kwamba kuna mkutano mkubwa unafanyika hapa Tanzania.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Tanzania ,Majaliwa amewataka Watanzania watumie fursa ya uwepo wa mkutano huo mkubwa kuendesha biashara zao na ujasiriamali. 

“Ziko fursa nyingi za uwepo wa mkutano huu. Kila mmoja atumie nafasi hii kuweza kuongeza na kuboresha kazi yake inayomletea uchumi,” amesema Majaliwa