Waziri Mkuu azindua jengo jipya hospitali ya Aga Khan

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwelekeza mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuhakikisha Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) unapata viwanja kwa ajili ya uwekezaji jijini humo.

Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa Hospitali ya Aga Khan ambayo pia ilihudhuriwa na Zahra Aga Khan, mtoto wa Mtukufu Aga Khan.

Sehemu ya hospitali iliyopanuliwa itakuwa ya kutolea mafunzo na rufaa na itakuwa na vitanda 170 kutoka 75 vilivyokuwapo awali.

Majaliwa alisema hivi sasa Serikali imehamishia shughuli zake Dodoma ambako wizara, taasisi na balozi mbalimbali zimepewa viwanja, michoro na ujenzi unaendelea.

Alisema kutokana na hatua hizo, uhitaji wa huduma za kijamii ni mkubwa.

“Ninawaalika nanyi kuja Dodoma kwa lengo la kupanua utoaji wa huduma za elimu, tiba na kadhalika. Fursa bado zipo na nilishamuelekeza mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ahakikishe taasisi kama hii ya Aga Khan zinapewa kipaumbele katika kupata viwanja kwa ajili ya uwekezaji,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na mtandao wa Aga Khan katika kuinua maisha ya Watanzania kijamii na kiuchumi hasa kupigania uboreshaji wa huduma za afya na elimu.

Waziri Mkuu alisema AKDN imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo hapa nchini tangu ilipoanza kuendesha shughuli zake zaidi ya miaka 100 iliyopita baada ya kuanzisha shule ya kwanza ya wasichana ya Aga Khan visiwani Zanzibar mwaka 1905.

Majaliwa alisema Hospitali ya Aga Khan ambayo imejengwa kwa viwango vya kimataifa itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha kuhudumia wagonjwa kutoka nchi za jirani, hivyo itaimarisha utalii wa tiba.

Aliipongeza AKDN kwa kupanua mtandao wa huduma za afya kwa kujenga vituo 35 nchini nzima na mpaka sasa 23 vimejengwa katika mikoa kumi na moja huku wananchi wakipata huduma kwa gharama nafuu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Zahra Aga Khan alisema mradi wa upanuzi wa hospitali hiyo umekwenda sambamba na usajili wa rasilimali watu wenye sifa na uwezo unaotambulika pamoja na hadhi za kimataifa.

Alisema hospitali hiyo itatoa huduma kwenye magonjwa ya moyo, saratani, mfumo wa fahamu na kinamama na watoto.

“Upanuzi huu utawawezesha Watanzania kupata matibabu ya daraja la juu wakiwa nyumbani, kwa hiyo itachochea utalii wa kimatibabu na pia kuhamasisha utalii huo katika ukanda huu,” alisema Zahra.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Hospitali ya Aga Khan ni muhimu katika sekta ya afya kwa sababu itatoa pia mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan na wahitimu wa kwanza wanatarajia kumaliza mwaka huu.