Wema Sepetu apanda kizimbani kwa dakika mbili

Muktasari:

Mwigizaji huyo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya kuchapisha video za ngono katika mtandao wa kijamii.


Dar es Salaam. Ilimchukua dakika mbili tu kwa mwigizaji maarufu wa filamu, Wema Sepetu kusimama katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu leo (Novemba 21).

Alipanda kizimbani saa 3:30 asubuhi na kushuka saa 3:32 asubuhi baada ya mahakama kuelezwa na upande wa mashtaka kuwa upelelezi wa shauri lake bado unaendelea na hivyo kesi hiyo isingeweza kusikilizwa kama ilivyopangwa.

Wema ameshtakiwa kwa tuhuma za kuchapisha na kusambaza picha za ngono katika mtandao wa kijamii wa Instagram Oktoba 15, lakini amekana kufanya kosa hilo.

Wakili wa Serikali, Jenifer Masuri alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Mwita Kasonde upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo shauri hilo lisingesikilizwa kama ilivyopangwa na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.

Wakili wa Wema, Ruben Simwanza hakuwa na pingamizi na ombi hilo na hivyo Hakimu Masonde kuahirisha kesi hadi hadi Desemba 12.

Msanii huyo alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza alipewa amri ya kutoweka video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye muelekeo huo katika ukurasa wa Instagram.

Mshtakiwa huyo alielezwa hayo na Hakimu Kasonde wakati akipewa masharti ya dhamana, ambayo ni kuwa na mtu mmoja aliyetakiwa kusini dhamana ya Sh10 milioni, masharti ambayo aliyatimiza.