Wizara ya afya yaeleza inavyowahudumia majeruhi ajali lori la mafuta Morogoro

Muktasari:

Wizara ya Afya nchini Tanzania imeeleza taratibu mbalimbali zinazofanywa kuhakikisha majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro wanapata matibabu stahiki

Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imeeleza taratibu mbalimbali zinazofanywa kuhakikisha majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro wanapata matibabu stahiki.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Agosti 10, 2019 na waziri wa wizara hiyo,  Ummy Mwalimu alipokuwa akielezea huduma mbalimbali za dharura zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro alipo majeruhi wa ajali hiyo.

Ajali hiyo imetokea leo baada ya lori la mafuta ya petroli kupinduka eneo la Msamvu na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo.

"Tumepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya moto iliyotokea leo Morogoro, Serikali kupitia wizara ya afya tupo kazini tayari Bohari ya Dawa (MSD) wapo njiani kupeleka dawa, vifaa na vifaa tiba vinavyohitajika haraka kwa magonjwa ya moto.”

"MSD wanapeleka vifaa tiba kama vile fluids, strong analgesics, Tetanus toxoid, burn creams, bed credos, gauzes, giving sets, urine bags, catheters  kwa ajili ya kuhudumia majeruhi,” amesema Ummy.

Amebainisha kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Zainab Chaula, mganga mkuu wa Serikali na timu ya wataalam kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wapo njiani kuelekea Morogoro ili kuongeza nguvu ya kuhudumia majeruhi.

"Ninawaombea majeruhi nafuu ya haraka. Pia ninatoa pole kwa ndugu, jamaa waliopoteza wapendwa wao," amesema Ummy.

Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema miili ya watu 60 waliokufa imehifadhiwa mochwari.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya amesema wamepokea miili 60 hadi leo saa 5:30 asubuhi na kwamba bado wanaendelea kupokea mingine.

“Majeruhi tuliowapokea hapa 52 wanaume na wanane ni wanawake. Tumelazimika kuwaomba madaktari na wauguzi kutoka hospitali na vituo vingine vya afya katika manispaa ya Morogoro kwa kuwa leo ni mapumziko,” amesema Lyamuya.

Akizungumzia kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Dk Kebwe amesema dereva wa lori alikuwa anakwepa bodaboda na kusababisha lori hilo kupinduka.

“Kwenye lori kulikuwa na watu watatu, dereva na kondakta na mwanamke mmoja. Dereva na huyo mwanamke wamebanwa watu walijitahidi kuwaokoa,” amesema Kebwe.

Amesema baada ya lori hilo kuanguka, mtu mmoja alitaka kuiba betri, wakati akifanya hivyo ukazuka moto na kusababisha maafa hayo.

Tukio hilo limetokea leo ambapo Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia miili iliyoungua ikiwa imelazwa pembeni ya barabara ya  Dar es Salaam-Morogoro wengi wakiwa ni madereva bodaboda na mamalishe wanaofanya shughuli zao hapo.

Saa 4 asubuhi leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema karibu watu 57 wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea saa mbili asubuhi.

Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kikuu cha mabasi Msamvu ukitokea Dar es Salaam.

Baadhi ya mashuhuda wamelieleza Mwananchi kuwa baada ya lori hilo kupinduka, watu walianza kuchota mafuta hayo.

Wamesema mmoja wa waliokuwa wakichota mafuta hayo alikuwa akivuta sigara, kwamba ndio chanzo cha mlipuko huo.

Abdallah Msambali amesema aliwaona waendesha bodaboda wakigombania kuchota mafuta kwa kutumia vyombo mbalimbali.

Miili ya waliofariki dunia imeondolewa eneo hilo na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Zimamoto na baadhi kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Leo asubuhi Kebwe wakati akihojiwa na wanahabari amesema, “Haijawahi kutokea maafa makubwa namna hivi Morogoro, lori lilikuwa limepakia mafuta ya petroli lilianguka pembeni mwa barabara hapa Msamvu na kuanza kuvuja mafuta ambayo yalisambaa umbali wa mita 100,” amesema Kebwe.

“Baada ya moto kudhibitiwa tutaangalia maiti nyingine zitakazokuwa zimebanwa na lori la mafuta. Madaktari wote waliopo Manispaa ya Morogoro tumeshawapanga hospitali ya Mkoa kutoa huduma kwa majeruhi, wagonjwa wenye nafuu tutawahamishia wodi nyingine kupisha hii dharura,” amesema Dk Kebwe.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi