Wizi wa magari watikisa Moshi

Saturday March 16 2019

 

By Daniel Mjema na Zainab Maeda,Mwananchi

Moshi. Wizi wa aina yake wa magari umeibuka mjini Moshi, lakini polisi wametoa maelezo kuwa unachangiwa na visa vya wanywaji wa pombe kuchezeana mchezo huo hatari.

Inadaiwa katika kipindi cha mwezi mmoja magari yasiyopungua matano yameibwa na kutelekezwa maeneo tofauti, lakini kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amedai ni mawili tu yaliyoripotiwa.

Vyanzo mbalimbali vya habari vinadai wizi huo umekuwa ukitokea zaidi katika kumbi za starehe na gari la karibuni kabisa kuibwa ni Toyota Pick na kutelekezwa maeneo ya Vijana kata ya Korongoni.

“Hao watu sijui ni akina nani wanaoiba hayo magari halafu wanayatelekeza. Unapomaliza kinywaji ukitoka unataka kuondoka ndio huoni gari lako. Baadaye unakuta limetelekezwa,” kilidai moja ya chanzo.

Mmoja wa wakazi wa Moshi ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alidai hata kama ni mchezo wa walevi lakini ni jambo la hatari pale wezi watakapokutana uso kwa uso na polisi wanaolisaka gari lililoibwa.

Hata hivyo, Kamanda Issah alipoulizwa na gazeti hili jana, alisema wimbi la wizi wa magari linaloendelea mjini Moshi linasababishwa na wamiliki au madereva wa magari kuwa walevi kupindukia.

Alisema matukio yaliyoripotiwa ni mawili lakini katika mahojiano ya awali na watu walioibiwa magari, walibaini baadhi yao walikuwa katika kumbi za starehe na wakiwa katika ulevi.

“Baadhi ya walioripoti kuibiwa magari walikuwa wanakunywa huko baa na unapowauliza funguo za gari ziko wapi hawajui ziko wapi. Wengi hawafungi magari wanayaacha tu bila kuyafunga,” alisema.

Kamanda Issah aliongeza kuwa, magari mawili yaliyopotea wiki iliyopita yalipatikana yakiwa yametelekezwa maeneo tofauti mjini hapa huku yakiwa salama bila kuibiwa chochote.

Hata hivyo, alisema huenda visa vya walevi ndio sababu ya magari kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuwataka wenye magari kuwa makini ili kuwaondolea polisi usumbufu na wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja.

Wizi uliozoeleka katika mikoa ya Kaskazini ukiwamo mkoa wa Kilimanjaro ni magari kuibwa nchini Kenya na kuingizwa mjini hapa au magari kuibwa mikoa mingine na kuuzwa mkoani Kilimanjaro.

Advertisement