Yajue mambo matatu ya kujifunza katika sikukuu hii kubwa ya matawi ya mitende

Askofu Jackson Sothenes Jackson

Muktasari:

  • Leo tunaadhimisha Jumapili ya matawi ya mitende. Wakristo wanaadhimisha siku hii kwa kufanya maandamano huku wakiwa wameshika miti ya mitende wakiimba na kumsifu Mungu.

Shalom Shalom wana wa Mungu. Jina langu naitwa Askofu Jackson Sosthenes Jackson kutoka Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam.

Leo tunaadhimisha Jumapili ya matawi ya mitende. Wakristo wanaadhimisha siku hii kwa kufanya maandamano huku wakiwa wameshika miti ya mitende wakiimba na kumsifu Mungu.

Mara nyingi wanapoadhimisha siku huu huwa wanarudia maneno ambayo waebrania walisema wakati wakimlaki Yesu kwa kutandaza nguo zo na matawi ya mitende wakisema ‘hosana hosana mwana wa Daudi uliye juu’.

Tukio hili linatokana na siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu. Tukisoma katika cha Injili ya Mathayo 21:9-10 neno la Mungu linasema “Makutano waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti wakisema ‘hosana mwana wa Daudi ndiye mbarikiwa ajaye wa jina la Bwana, Hosana juu mbinguni’ hata alipoingia Yesusalemu mji wote ukataharuki watu wakisema ni nani huyu? Makutano wakasema huyu ndiye yule nabii Yesu Mnazareti wa Galilaya”.

Jambo la msingi la kutafakari kabla ya kuangalia sisi jamii na kanisa la sasa sikukuu ya mitende inamaana gani kwetu, ni nikuangalia maana na mazingira ya wayahudi yaliyowasukuma wao kuadhimisha siku ile kwa kutamka maneno yale wakirudia ‘Hosana mwana wa Daudi uliye juu”.

Neno ‘Hosana’ ni la kiebrania likimaanisha ‘okoa sasa’. Kama waliimba okoa sasa kwanini waliutaka wokovu?

Naomba ifahamike kwamba wakati Yesu akiwa duniani kufanya huduma yake kutoka mwaka mwaka 63 kabla ya Krsto, wayahudi walikuwa chini ya utawala wa warumi.

Kwa muda mwingi walitarajia wokovu na kupata mfalme atakaye watawala na kuwaweka huru.

Wanapomuona kristo wanaona kama masihi aliyekuja kuwakomboa na kuwatoa katika mikono ya watesi wao.

Kwa hiyo wimbo ule na alama ya matawi ya matende ilikuwa ni ishara ya kumuona Kristo kama mfalme atakaye weza kuwaokoa katika mikono ya waliowatesa na kuwatawala kwa muda mrefu.

Kwetu sisi wa leo, tunapoadhimisha sikukuu hii yapo mambo matatu ambayo tunapaswa kuyaona na kuyatafakati kama kanisa na jamii.

Kwanza ni namna gani tunampa nafasi Kristo katika maisha yetu.

Wayahudi waliacha shughuli zao na ratiba zao mbalimbali wakimlaki Yesu na kumshangilia kwa matawi ya mitende wakitandaza njiani na kumpa nafasi Kristo kama mtawala aliyestahili kupewa heshima na kuweza kuwatoa kwenye mateso na vifungo.

Kwetu sisi kama kanisa la sasa tunaweza kujiuliza, tunampa nafasi gani Yesu kristo kama mtawala wa maisha yetu?

Je, tunamuona kama mtawala wa maisha yetu au tumeruhusu fikra zetu na mawazo yetu yaweze kutawala maisha yetu?

Sikukuu hii itupatie nafasi kama Wayahudi walivyotandaza matawi ya mitende, nasi tutandaze mioyo yetu kwa Kristo ili aweze kutawala katikati ya maisha yetu.

Unapoandamana na tawi la mtende katika mkono wako, kristo unamuona nani katika moyo wako?

Kristo aonekane kuwa ni mtawala ili atusaidie tuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Kama kanisa pia baada ya kuona uweza, nguvu na utawala wa Kristo katika maisha yetu kuna jambo la pili la kujifunza katika sikukuu hii.

Jambo hilo la pili ni kuomba wokovu wa kristo utawale katika jamii yetu. Tunaishi katika jamii inayohitaji msaada wa Mungu katika maeneo mengi.

Tunashukuru kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali yetu, na watawala na viongozi waliopewa dhamana katika nchi yetu.

Lakini yapo mambo tunamuhitaji Kristo kama wayahudi walivyosema ‘okosa sasa’ Kristo afanyike hosana katikakati ya mengi ambayo jamii yetu inahitaji.

Tunahitaji atuokoe katika vitendo vya rushwa, ufisadi na mambo yanayokwamisha maendeleo ya jamii na taifa letu.

Pia atusaidia kuliwezesha kutoka katika kila aina ya mazingira yenye kufanya binadamu tushindwe kufikia furaha na maendeleo tuliyobarikiwa aidha kwa wachache ambao bado hawajakubali kuruhusu mioyo yao kufanyika baraka na kuwatumikia watanzania uaminifu bila kutawaliwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Kristo aliye wokovu wetu aiokoe jamii yetu na aliokoe kanisa lake pia.

Jambo la tatu la kujifunza katika sikukuu ya matawi ya mitende ni amani. Tunamwona Kristo akiingia Yerusalemu kama mfalme lakini akiwa amepanda punda.

Punda ni mpole na mnyenyekevu. Punda ni mnyama wa amani kwa hiyo Kristo kuingia Yesusalemu aliashiria juu ya ufalme wa amani kwamba yeye ni amani yetu.

Tunapoadhimisha sikukuu hiyo ya mitende tuombee amani katika nchi yetu, familia zetu na nchi jirani kipekee sana yanayoendelea Afrika Kusini kuwaua na kuwafukuza waafrika wenzao na kusahau historia za waasisi waliotuunganisha.

Pamoja na kwamba tunawasihi viongozi wetu wachukue nafasi zao kuleta amani lakini pia sikukuu hii ya mitende tuchukue nafasi ya kuiomba amani ya kristo itawale kwenye mioyo yetu, familia zetu, jamii yetu na nchi zetu. Amen. Mungu akubariki