Zanzibar yatakiwa kutafuta soko la biashara nje ya Tanzania

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamo wa pili wa Rasi Zanzibar Mohamed Aboud Mohamed akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na wajumbe wa kamati ya uongozi ya mfuko wa maendeleo Tasaf.Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Serikali ya Zanzibar imeshauri kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali nje ya Tanzania ili kuongeza uchumi wa visiwa hivyo.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kutafuta soko la kibiashara nje ya Tanzania kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar baada ya soko la Tanzania bara kuwa ni gumu kupatikana.

Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti ya Baraza la wawakilishi, Mohamed Said Mohamed almesema hayo leo Jumanne Juni 25,2019  katika mjadala wa bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2019-2020 ya Sh1.4 trilioni unaendelea kujadiliwa na wajumbe wa baraza hilo.

Amesema Serikali imeshafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha wanafanya mazungumzo na wenzao wa Serikali ya Muungano juu ya suala la biashara kati ya Zanzibar na Tanzania bara, lakini inaonekana mazungumzo hayo yameshindwa kupatiwa ufumbuzi wenye tija ni vyema sasa kwa Serikali kuangalia njia mbadala wa soko la Tanzania bara.

Amesema huu si wakati wa kuwaacha wafanyabiashara kulazimisha kulitumia soko la Tanzania bara tu, bali ni wakati kwa Serikali kuyasaka masoko kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Kenya, Comoro na sehemu nyengine mbalimbali ili kuona wanakuwa kiuchumi.

Mohamed amesema kufanya hivyo kutawawezesha wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa Zanzibar kuendelea kiuchumi pamoja na kuipatia kodi mbalimbali Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maslahi ya maendeleo ya watu wake.