Zitto ajibu hoja tatu za Msajili

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Barua hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Msajili anapotaka kufuta usajili wa chama cha siasa anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa chama hicho.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amefafanua mambo matatu yaliyomo katika barua ambayo chama chake imeandikiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Pamoja na ufafanuzi huo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema, “sisi tumemuandikia barua na tumempa nafasi ya kuleta utetezi, maelezo, ufafanuzi kwa maandishi, busara ni kufanya kama tulivyomuelekeza, hayo ni mambo ya kiofisi na yatamalizwa kiofisi kwa mujibu wa sheria na maelekezo.”

Juzi, Ofisi ya Msajili ilieleza nia yake ya kukifutia usajili chama hicho na kukipa siku 14 kuanzia jana, kuwasilisha maelezo ya kwa nini kisifutiwe uanachama wa kudumu.

Barua hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Msajili anapotaka kufuta usajili wa chama cha siasa anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa chama hicho.

Imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na chama hicho kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria vya kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.

Pia, chama hicho kinatuhumiwa kutumia dini baada ya mashabiki wake kuonekana mitandaoni wakipandisha bendera ya ACT Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbir), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

Mbali na hatua hizo, ofisi ya msajili imesema chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 kinakabiliwa na adhabu nyingine ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.

Kuhusu ukaguzi

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Zitto alisema tuhuma kuhusu kutowasilisha hesabu za mwaka 2013/14 hazina ukweli wowote.

Zitto alisema wajibu wa chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na Hesabu za Serikali (CAG) na kwa kulitambua hilo, waliwasilisha hesabu za mwaka 2013/14 kama ilivyotakiwa.

“Chama chetu kilianzishwa na kupata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuisha yaani Juni 30, 2014. Kwa kutumia kanuni za kimataifa za hesabu na kwa ushauri wa CAG, chama chetu kilielezwa kinaweza kuunganisha hesabu za mwaka 2013/14 na za 2014/15 katika ripoti moja, hili ni jambo la kawaida kabisa katika kanuni za uhasibu, inaruhusiwa kuunganisha hadi miezi 18,” alisema Zitto.

Alisema kabla ya kufanya hivyo, walimwandikia Msajili barua mbili ya Januari 22 na 29, 2015 naye akajibu kuridhia hesabu hizo kuunganishwa kwenye barua ya Februari 16, 2015.

“Taarifa zote hizi zipo kwa CAG. Msajili angekuwa na nia njema, angeweza kuuliza na angepewa taarifa sahihi. Chama cha siasa wajibu wake ni kuwasilisha hesabu kwa CAG na si kukagua hesabu zake chenyewe. Tulitimiza wajibu wetu, CAG alitimiza wajibu wake, chama chetu hakuna mwaka hakijawasilisha hesabu zake,” alisema.

Alisema chama hicho kina hati safi za ukaguzi na Msajili anajua kuwa ndicho chama pekee chenye hati safi mezani kwake.

Kuchoma bendera

Kuhusu kuchoma bendera za CUF alisema Msajili katika barua yake, ameonyesha kutokuwa na uhakika kama kweli waliofanya hivyo ni wanachama wa ACT Wazalendo.

Alisema chama chake kina orodha ya wanachama waliopewa kadi, “Msajili alipaswa ajiridhishe anaowatuhumu ni wanachama wa ACT Wazalendo, kabla ya kutuandikia barua. Nina uhakika hawezi kwenda mbele ya mahakama kuthibitisha hilo.”

Kutumia neno ‘Takbir’

Kiongozi huyo alisema ni jambo lililowashangaza kushutumiwa kutumia neno Takbir akisema ACT Wazalando ni chama cha watu wote wala hakibagui dini.

Alisema Katiba na kanuni za chama hicho inaonyesha wazi kuwa hawafungamani na dini yoyote ndiyo maana wameruhusiwa kufanya shughuli za siasa.

“Tunafahamu Watanzania wana dini zao, lakini kutumika kwa baadhi ya maneno ya dini zao katika mikutano au mikusanyiko ya watu haina maana ni udini, viongozi wote hufungua hutuba zao kwa kusema Bwana Yesu asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo na Assalamu Alaykum hatuamini kama kusema hivyo ni udini,” alisema Zitto.

Alisema jambo hilo wanawaachia wanazuoni na viongozi wa dini walifafanue kama Mwislamu akisema takbir ni udini, “Sheikh Mkuu atoe fatua kuhusu neno hilo,” alisema Zitto.

Alisema watu wote wanaopenda demokrasia walione suala hilo kuwa linaweza kuharibu amani.

Alisema amani na utulivu uliopo ni kwa sababu wananchi wana chaguo, kwamba wakichoshwa na CCM watakwenda Chadema au CUF au NLD au Chaumma na kwingineko.

“Nawaasa wanachama wote wafanye shughuli zao za chama kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa kutimiza matakwa yote ya kikatiba.

“Suala hili lisiwaogopeshe linashughulikiwa ikiwamo kujibu barua kwa kuambatanisha na vielelezo vyote vilivyopo,” alisema Zitto.