Zitto mgonjwa, kesi yake yakwama, hakimu atoa neno

Muktasari:

  • Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameshindwa kufika mahakamani leo Jumatatu kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni mgonjwa.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni mgonjwa.

Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu katika kesi ya uchochezi, inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya ugonjwa wa Zitto, zimetolewa leo Jumatatu Machi 11, 2019 na wakili wake, Steven Mwakibolwa, baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa hawamuoni mshtakiwa mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakamani hiyo, Huruma Shaidi, kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa ushahidi, lakini mshtakiwa hayupo mahakamani hapo na upande wa mashtaka hawana  taarifa zake.

“Upande wa mashtaka tayari tunaye shahidi mmoja ambaye ni ASP Shamila Mkoma na tupo tayari kuendelea na ushahidi, lakini kwa bahati mbaya hatumuoni mshtakiwa mahakamani hapa, wakili wake yupo hapa atatuambia alipo mshtakiwa,"amedai Simon.

Simon baada ya kueleza hayo, Wakili Mwakibolwa, anayemtetea Zitto amedai mteja wake ni mgonjwa na leo, ameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

"Nimepewa taarifa asubuhi hii kuwa Zitto ni mgonjwa, lakini amekuja shemeji yake mahakamani hapo kutoa taarifa hivyo, ataieleza mahakama juu ya afya ya Zitto," amedai Mwakibolwa.

Baada ya Mwakibolwa kueleza hiyo, ndugu wa Zitto, aitwaye Vicent Kasara amedai kuwa mshtakiwa ni mgonjwa.

Kasara ambaye ni shemeji yake Zitto, amedai amepigiwa simu asubuhi na dada yake (mke wa Zitto) na kupewa taarifa kuwa shemeji yake ni mgonjwa, hivyo aje mahakamani kutoa taarifa.

"Nimepewa taarifa asubuhi na dada yangu kuwa shemeji yangu ni mgonjwa, ila sielewi anaumwa nini," amedai Kasara.

Baada ya Kasara kueleza hayo, Hakimu Shaidi alimhoji shemeji yake Zitto, “kama shemeji yako anaumwa na hujui anaumwa nini na wala hujui yuko wapi? Sasa unakuja  kutuambia mshtakiwa anaumwa bila maelezo ya kujitosheleza.

"Tusitafutane maneno hapa, mdhamini au ndugu unapaswa uje utoe taarifa iliyokamilika, kama mshtakiwa anaumwa, anaumwa nini? Yupo sehemu gani? Si unatoa taarifa ambazo hazijakamilika," amesema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi amemtaka shemeji wa Zitto, kufuata taratibu zinazotakiwa, wakati anawasilisha taarifa zinazohusu mshtakiwa.

"Unatakiwa kufuata taratibu za kutoa taarifa sahihi kama sheria zinavyotaka, kwa sababu hapa tukisema na sisi tukaze vyuma, vitakuwa vigumu zaidi," amesema Hakimu Shaidi na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 9, 2019 itakapoendelea na ushahidi.

Zitto alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018.

Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Moja ya mashtaka hayo, Zitto anadaiwa kuwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua"

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa ni maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.