Zuio mifuko ya plastiki lawaibua wanamazingira, wenye viwanda

Pengine Watanzania walio wengi wameanza kujiuliza maisha yatakuwaje bila ya mifuko ya plastiki waliyozowea kuitumia kubebea bidhaa mbalimbali.

Hali itakuwaje baada ya Mei 31 siku ya mwisho kwa Mtanzania kuonekana mtaani amebeba mifuko ya plastiki kwani Juni Mosi mifuko hiyo haitakiwi kuonekana.

Ni dhahiri wengi bado wako katika tafakari kufuatia agizo hilo la kupiga marufuku mifuko ya plastiki lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aprili 9, mwaka huu akiwa bungeni mjini Dodoma.

Marufuku au zuio hilo limepokewa kwa mikono miwili na wanamazingira ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipigia kelele matumizi ya mifuko ingawa kwa wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara kwao umekuwa mtihani, wanahofu kupoteza ajira na viwanda kufungwa.

Abdallah Issa ni meneja wa kiwanda cha Dar es Salaam Oceanic Development (DOD) ambacho kinafanya biashara ya bidhaa za plastiki, anasema agizo hilo kwao maana yake ni kujiandaa kupata hasara.

“Hivi ninavyozungumza tuna mwezi mmoja kama na nusu hivi wa kumaliza malighafi tuliyonayo na bidhaa zetu, inawezekana vipi katika kipindi hiki kifupi,’’ anasema Abdallah.

Anasema kwamba anatambua kilio cha bidhaa za plastiki na kukiri majirani Kenya, Rwanda na Zanzibar wameshachukua hatua lakini anasisitiza suala la maandalizi na watu kupewa muda wa kutosha.

Anaongeza kuwa huko nyuma yaliwahi kufanyika mazungumzo kuhusu mifuko ya plastiki yaliyohusisha wadau mbalimbali lakini suluhisho halikufikiwa.

“Kuna waliozungumzia katani na hapo likaja swali je ipo ya kutosha kuzalisha vifungashio ambavyo vitachukua nafasi ya bidhaa za plastiki?’’ Alihoji.

“Sisi tulichotaka ni majadiliano lakini badala yake tumesikia agizo limetolewa, hatuna tatizo lakini tulihitaji kuwe na sera na makubaliano ya kulifanyia kazi jambo hili,’’ aliongeza.

Akizungumza na gazeti la The Citizen ambalo ni gazeti dada la Mwananchi, mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Bidhaa za Plastiki Tanzania (PMAT) Mushtak Walij naye alizungumzia hofu ya kupata hasara kwa wenye viwanda.

Walij anasema kwamba Serikali ilitakiwa kuwapa muda wa miezi sita hadi saba ili waweze kuuza malighafi walizoagiza na zile walizozalisha nchini.

Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma, siku moja baada ya agizo la Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) January Makamba alisema kwamba uamuzi huu si wa kushtukiza bali ni mpango wa muda mrefu ulioshirikisha wadau wote.

Makamba pia alisema kwamba si mifuko yote ya plastiki inazalishwa na viwanda vya Tanzania bali sehemu kubwa ni ya viwanda vya nje karibu asilimia 80, hivyo kama ni kuua viwanda tatizo litakuwa kwa viwanda vya nje zaidi.

Kilio cha Walij na Abdallah kinachowakilisha wenye viwanda vya bidhaa za plastiki nchini, pia kilisikika Kenya wakati nchi hiyo ilipotangaza marufuku ya matumizi ya mifuko hiyo, Agosti mwaka 2017.

Chama cha Wazalishaji sekta ya Viwanda Kenya (KAM) kililalamikia tatizo hilo kwa madai kwamba tatizo si mifuko ya plastiki bali ni tabia za watumiaji katika kuhifadhi mazingira.

Zaidi ya hilo KAM pia walilalamikia hasara katika viwanda hivyo kwa watu kupoteza ajira na hata viwanda kufungwa kutokana na kubadili bidhaa.

Kenya ilivyofanikiwa

Pamoja na malalamiko hayo, nchini Kenya hasa jiji la Nairobi ikiwa ni takriban miaka miwili sasa marufuku hiyo imefanikiwa, mifuko ya plastiki haipo, vifungashio rafiki kwa mazingira ndivyo vilivyochukua nafasi ya mifuko ya plastiki.

Mafanikio ya marufuku ya Kenya yanatajwa kuchangiwa na sheria kali iliyowekwa, mtu akikutwa anauza, kuzalisha au kutumia mifuko ya plastiki adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka minne jela au faini inayotajwa kufikia hadi Sh80 milioni za Tanzania.

Wakati wenye viwanda wakiwa na malalamiko hayo, kwa wadau wa mazingira agizo la Waziri Mkuu ni mfano wa neema waliyokuwa wakiisubiri muda mrefu.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Mabadiliko ya Tabianchi (Forum CC), Rebecca Munna anasema kwamba wameupokea kwa mikono miwili uamuzi wa Serikali ambao walikuwa wakiusubiri kwa miaka mingi.

Rebecca anasema kwamba mifuko ya plastiki madhara yake si katika uharibifu wa mazingira tunayoishi kwa maana ya ardhi kwa kuwa mifuko hiyo haiozi, bali madhara hayo yamekwenda hadi kwa viumbe wa majini.

Samaki na viumbe wengine wanakufa kwa sababu takataka za plastiki zimekuwa nyingi katika bahari, mito na maziwa na wanyama wengine wanaofugwa kama ng’ombe wako wanaokula mifuko hiyo na wengine hata kufa.

Akizungumzia hofu ya wenye viwanda kupoteza ajira na soko lao, Rebecca anasema hawapaswi kuwa na hofu hiyo badala yake wanatakiwa kubadili teknolojia na kuubadili uamuzi wa Serikali kuwa fursa kwao.

“Wanatakiwa kugeukia teknolojia rafiki kwa mazingira, wakifanya hivyo ajira zitaongezeka na zaidi ya hilo watakuwa wameokoa gharama zinazotokana na uharibifu wa mazingira ambazo pia ni kubwa,’’ anasema Rebecca.

Hoja za Rebecca zinaungwa mkono na Profesa Honest Ngowi, mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam ambaye anasema wenye viwanda wanatakiwa kugeukia fursa hii ili kuzalisha mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Anasema tatizo la mifuko ya plastiki haiozi na madhara yake katika mazingira ni makubwa hivyo agizo la Serikali ni zuri kwani linaipeleka nchi katika uchumi wa kijani.

Zaidi ya hilo, Profesa Ngowi anasema agizo la Serikali ni fursa kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha mifuko rafiki kwa mazingira ambao wanatakiwa kuongeza uzalishaji kwa kuwa wana uhakika wa soko.

Hata hivyo Profesa Ngowi anakiri kwamba suala la muda uliotolewa ni muhimu kujadiliwa kwa wenye viwanda au wajasiriamali wenye akiba ambayo haijauzwa ili kupata mwafaka utakaowaepusha na hasara.

“Ni lazima wazalishaji wabadili teknolojia, wageukie iliyo rafiki kwa kuzalisha mifuko ya aina nyingine,’’ alisema ingawa anakiri kwamba hana uhakika kama teknolojia ya wazalishaji hao inaweza kubadilishwa.

Kuhusu hofu ya wenye viwanda, mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet) John Chikomo anasema kwamba wenye viwanda hawatakiwi kulalamika badala yake waje na bidhaa ambazo hazina madhara kwenye mazingira.

“Tangu tukiwa wadogo tulitumia mifuko ya karatasi, kuna iliyotengenezwa viwandani na mingine ilitengenezwa na watu binafsi, kwa hiyo naona wanaweza kuchangamkia fursa hiyo,’’ anasema Chikomo.

Chikomo pia anasema kwamba tatizo la mifuko ya plastiki si la Tanzania pekee bali ni duniani kote, kila nchi imekuwa ikilalamikia mifuko ya plastiki, ina madhara kwenye ardhi, kwa wanyama na viumbe wa baharini.

Amesema kwamba kuna wanyama wanaoathirika baada ya kula plastiki lakini kwa samaki na hali ya ustawi wa bahari, mito, maziwa na vyanzo vya maji mifuko hii imekuwa chanzo cha tatizo kubwa.

“Kuna walioweka tozo ili kupunguza matumizi ya mifuko hii lakini haikusaidia sana hivyo uamuzi wa Tanzania tunauunga mkono na tuko tayari kutoa elimu kwa jamii,’’ anasema.