Kutekwa kwa Mo Dewji, Serikali yasema itafunga CCTV miji mikubwa

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha wanafunga kamera katika miji mikubwa ii kujiimarisha katika ulinzi

Arusha. Serikali inatarajia kusambaza kamera maalum za CCTV katika miji mikubwa na mikoa iliyoko karibu na mipaka ya nchi kwa lengo la kujizatiti katika masuala ya ulinzi ikiwemo matukio ya utekaji. 

Hayo yamesemwa leo Oktoba 14, 2018 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kwenye ziara ya kutembelea vitengo vya wizara yake vilivyoko jijini humo.

Masauni amesema mazingira ya utendaji kazi wa polisi yamekuwa na changamoto nyingi ambazo baadhi yake zinakwaza utekelezaji wa majukumu yao hivyo Serikali imeamua kuwaongeza nguvu ili kurahisisha majukumu yao.

“Matumizi ya teknolojia hayaepukiki kwa dunia ya sasa, hivyo Serikali tumejipanga na tutaanza kutekeleza hivi karibuni usambazaji wa kamera za CCTV katika miji mikubwa na mikoa iliyoko mipakani mwa nchi.”

“Haya matukio ya utekaji ni sifa mbaya sana ila sitaki kulielezea sana maana jana (juzi) Waziri wa Mambo ya Ndani (Kangi Lugola) amezungumza mengi ikiwemo mafanikio ya jeshi la polisi, ila hili la mfanyabiashara ‘Mo (Mohamed Dewji) limechukua sura kubwa hadi duniani kutokana na umaarufu wake na linatisha hata watalii lakini niseme Serikali ina mikakati ya kutokomeza hili,” alisema Masauni.

Masauni amewaonya wanasiasa wanaotumia matukio yanayojitokeza nchini kujipatia umaarufu kwa kusingizia baadhi ya mamlaka za Serikali au taasisi za watu.