Lema: Serikali ikubali vyombo vya nje kuchunguza kutekwa kwa Mo Dewji

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema 

Muktasari:

Lema ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari akibainisha kuwa hiyo ndio njia pekee ya Serikali kujiondoa katika lawama

 


Dar es Salaam. Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema amesema njia pekee ya Serikali kujiondoa katika lawama tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ni kuruhusu vyombo vya nje kufanya uchunguzi.

Lema ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Chadema Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mbunge huyo wa Arusha Mjini amesema haitakuwa aibu kwa Serikali kuhusisha vyombo vya nje kwa kuwa hata mataifa yaliyoendelea huwa yanaomba msaada inapobidi.

Amesema kwa mazingira ya eneo ambalo Mo Dewji ametekwa kuna ulinzi wa hali ya juu, kushangazwa na mfanyabiashara huyo kutopatikana hadi sasa.

Lema pia amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutozuia watu kujadili tukio hilo.

Jana,  familia ya Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40, ilitangaza dau la Sh1bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.

Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi Oktoba 11, 2018 saa 11:30 alfajiri wakati akiwa Hoteli ya Colosseum na hadi leo saa 5:40 asubuhi hakuna taarifa zozote za watekaji, lengo la kumteka wala fununu za alikohifadhiwa.