Lissu: Natamani kuonyesha ishara ya vidole viwili

Muktasari:

  • Akiwa hospitali jijini Nairobi, Lissu amesema anatamani kuonyesha vidole viwili

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema hali ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu inaendelea vizuri na anatamani apate nafuu na kunyoosha vidole viwili (ishara ambayo hutumiwa na Chadema).

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum leo Jumatano jioni jijini Dar es Salaam, Mchungaji Msigwa amesema kwa kipindi chote hicho Lissu hakuwa akila na hali yake imebadilika ukilinganisha na alivyokuwa hapo awali lakini hivi sasa anakula vitu laini.

“Leo kabla sijaanza safari ya kuja (kurudi Dar es Salaam) amenitania sana kwa kusema anatamani apate nafuu na kuonyesha alama ya vidole viwili,” amesema Mchungaji Msigwa.

Msigwa ameeleza wanaendelea kujadiliana na madaktari ili kuangalia uwezekano wa kumpeleka nchi nyingine kwa ajili ya matibabu zaidi.

Amesema Lissu anaangaliwa na madaktari 10 kila mmoja akishughulika na eneo lake ili kuhakikisha hali yake inatengemaa.

“Miongoni mwa mambo anayoyarudia ni kututaka kuendelea kupambana, kupaza sauti kuikomboa nchi, ”amesema Msigwa.