Ma-admin makundi ya Whatsapp waonywa

Muktasari:

Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA)imesema wasimamizi wa makundi ya Whatsap wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kushindwa kuwajibisha wachangiaji wanaotoa maudhui yasiyofaa na kuwa wao wanawajibika kulinda maadili mema kwa wanachama wao

 

Bukoba.Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imewaonya wasimamizi 'Admin' wa makundi ya Whatsapp yaliyoundwa kwenye simu za mkononi kwa kutosimamia maadili ya wanachama.

Makundi hayo ambayo huanzishwa kwa lengo mahususi yanatumika kama majukwaa ya mijadala,maelekezo ya kazi hata malumbano huku aliyeunganishwa akiwa na uhuru wa kujitoa kwenye kundi.

Onyo la TCRA dhidi ya wasimamizi wa makundi hayo limetolewa leo Oktoba 5 mjini Bukoba na ofisa wa mamlaka hiyo, Francis Mihayo wakati wa semina kwa viongozi wa mkoa wa Kagera.

Amesema kuwa 'admin'wanawajibika kusimamia maadili ya wanachama wao kwa kuchukua hatua ya kuwaondoa ikiwa watatoa maudhui ambayo hayana mtazamo mzuri kwenye jamii kama lugha isiyofaa.

Amewataka wasimamizi hao wa makundi hayo kutoogopa kuwaondoa wanachama wao wanaokiuka maadili kwa kuwa wao kama wasimamizi wanaweza kuchukuliwa hatua na mamlaka hiyo.

Mamlaka hiyo imekutana na viongozi wa ngazi tofauti kutoka wilaya zote za mkoa wa Kagera ambapo umetolewa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa kuondolewa kwa chaneli za ndani kwa baadhi ya ving’amuzi.