Maalim Seif afunguka kuhusu Profesa Lipumba

Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

Muktasari:

Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Zanzibar/Mtwara. Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye amekuwa kimya kuzungumzia sakata linaloendelea ndani ya chama hicho likimuhusisha Profesa Ibrahim Lipumba, jana aliondoa ukimya na kueleza kuwa kinachoendelea ni mpango ulioandaliwa wa kuvuruga jitihada za chama hicho za kudai haki, lakini hautafanikiwa.

Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Maalim Seif alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake fupi kwa mamia ya waumini na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika Msikiti wa Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.

CUF iko kwenye mvutano wa uongozi kutokana na Profesa Lipumba kushika ofisi kuu za chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam akisema kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutoa msimamo na maoni ya ofisi yake kuhusu sakata hilo.

Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana, akipinga chama hicho kuendelea kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya vyama vinne vinavyounda umoja huo kumpitisha Edward Lowassa kuwa mgombea wao wa urais.

Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa Lipumba alimuandikia barua katibu mkuu akitaka atengue barua yake ya kujiuzulu, lakini Mkutano Mkuu wa chama hicho ulijadili suala hilo na kuazimia kukubaliana na kujiuzulu na baadaye Baraza Kuu kupitisha uamuzi wa kumvua uanachama.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi