Maandamano mtandaoni yawaponza watatu Tanga

Muktasari:

Aliwataka wakazi wa Tanga kuondoa hofu kwamba kutakuwapo na maandamano hayo kwa sababu jeshi limejiandaa kumshughulikia kila atakayethubutu kuandamana.

Tanga/Dar. Vuguvugu la maandamano yanayoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii kufanyika Aprili 26, limesababisha watu watatu jijini Tanga kushikiliwa na polisi wakituhumiwa kuyaratibu.

Hata hivyo, Polisi imesema hakuna maandamano yoyote yaliyoruhusiwa kufanyika siku hiyo na kutahadharisha kuwa yeyote atakayeandamana asije akawalaumu askari au Serikali kwa sababu atakuwa ‘amelamba sumu’.

Akizungumza na Mwananchi jana, kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema wanaoshikiliwa walikamatwa maeneo tofauti jijini Tanga baada ya kufuatiliwa na kubainika kuwa wanahamasisha maandamano kwenye mitandao ya kijamii.

“Tayari watu watatu waliohamasisha maandamano haya kupitia mitandao ya kijamii tunawashikilia na wapo wengine ambao tunawafuatilia, tutawakamata wakati wowote kwa kuwa tunazo taarifa zao na mbinu wanazotumia,” alisema Kamanda Bukombe

Aliwataka wakazi wa Tanga kuondoa hofu kwamba kutakuwapo na maandamano hayo kwa sababu jeshi limejiandaa kumshughulikia kila atakayethubutu kuandamana.

Machi 21, Polisi Mkoa wa Dodoma iliwakamata na kuwashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kwenye mitandao ya kijamii Aprili 26.

Zuio la mkutano

Tishio hilo la maandamano limesababisha Polisi katika Wilaya Masasi, Mtwara kuzuia ziara ya mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe katika Kata ya Lukuledi kwa maelezo kuwa jeshi hilo sasa lipo katika hali ya tahadhari (standy by) kujiandaa na sherehe za Muungano, Aprili 26.

Alipoulizwa iwapo hali hiyo ya tahadhari ni kwa nchi nzima, msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa alisema kila kiongozi ndani ya jeshi hilo kuanzia IGP hadi kwa kiongozi ndani ya wilaya (OCD) ana mamlaka yake katika eneo lake.

“Suala si la kitaifa au vipi, jua tu kuwa kila mmoja ana mamlaka katika eneo lake, kama jambo limetangazwa mkoani waulize viongozi wa polisi katika mkoa husika, kama yeye ameelezea sababu za kufanya hivyo ndizo hizo, huku unauliza nini tena,” alihoji Mwakalukwa.

Katika barua ya OCD, Moshi Sokoro kwa Mwambe ambayo Mwananchi imeiona ilieleza kuwa mkutano huo umezuiwa kutokana na shughuli hiyo ya kitaifa kwa sababu hakutakuwa na askari wa kutosha kuratibu ziara na kusimamia mkutano huo.

Aprili 20, Mwambe aliomba kufanya mkutano akiambatana na viongozi wengine wa Chadema ngazi ya taifa, Kanda ya Kaskazini, mkoa na wilaya. Siku iliyofuata alijibiwa kuwa ziara hiyo imekataliwa.

Nakala ya barua hiyo inaonyesha ilipelekwa kama taarifa kwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara; mkuu wa upelelezi mkoa huo; mkuu wa Wilaya ya Masasi na mkuu wa Usalama wa Taifa wa Wilaya ya Masasi. Mpelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya ya Masasi alipewa nakala kwa ajili ya utekelezaji.

Polisi watano wajeruhiwa Tanga

Katika hatua nyingine, askari watano wa kitengo cha upelelezi Tanga wamejeruhiwa baada ya gari la Polisi aina ya Land Rover 110 kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania lenye trela wakati magari hayo yakipishana katika barabara ya Tanga-Horohoro.

Kamanda Bukombe alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa saba mchana karibu na daraja la Mto Utofu wakati askari hao wakielekea kwenye majukumu yao ya kikazi. Askari hao ni Sajenti Henry, Konstebo Jafary dereva wa gari la Polisi, Konstebo Barnabas, Konstebo Fatuma na Konstebo Obed.

Alisema dereva wa lori alikimbia na polisi wanaendelea kumsaka.