Madai watu kufia mikononi mwa polisi yaibua hoja sheria ya vifo tata kutumika

Frank Kapange enzi za uhai wake

Muktasari:

Matukio ya watu kudaiwa kufa mikononi mwa polisi kwa kipigo au matumizi ya nguvu yaliyopitiliza yamewafanya pia wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wadai kuanza kutumika kikamilifu kwa sheria za uchunguzi wa vifo vyenye utata ili kuthibitisha ukweli.


Dar es Salaam. Utaratibu wa Jeshi la Polisi kujivika jukumu la kuchunguza vifo linavyotuhumiwa kusababisha na kutotumika kwa sheria ya kuchunguza vifo vyenye utata, unaweza kuwa mwanzo wa ‘kuzika’ ukweli mwingi kuhusu matukio ya aina hiyo.

Mwaka 1980, Tanzania ilitunga Sheria ya Kuchunguza Vifo (Inquest Act, 1980) ambayo inatoa mamlaka kwa Waziri wa Katiba na Sheria kuanzisha mahakama ya kuchunguza kifo chochote chenye utata (coroner’s court) katika eneo husika kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.

Kutotumika kwa sheria hiyo ya uchunguzi huru wa vifo vya watu wanaofia mikononi mwa jeshi hilo na vingine vyenye utata, kunaibua maswali mengi ni kwa nini mamlaka zinaiweka kando sheria hiyo.

Matukio ya watu kudaiwa kufa mikononi mwa polisi kwa kipigo au matumizi ya nguvu yaliyopitiliza yamewafanya pia wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wadai kuanza kutumika kikamilifu kwa sheria za uchunguzi wa vifo vyenye utata ili kuthibitisha ukweli.

Matukio yenyewe

Katika miezi ya karibuni, matukio kadhaa ya watu waliokamatwa na polisi wakiwa wazima na baada ya muda wakaripotiwa kupoteza maisha mikononi mwa walinda usalama hao au hospitali kwa madai ya kupigwa na kuteswa, yameanza kushika kasi. Wapo pia waliouawa kwa kupigwa risasi katika mazingira yaliyodaiwa kuibua utata.

Mara zote matukio ya aina hiyo yanapotokea, Jeshi la Polisi limekuwa likiunda kamati za kuchunguza lakini matokeo ya uchunguzi yamekuwa hayatolewi na malalamiko ya ndugu na jamaa huishia hewani.

Matukio hayo yanahofiwa kujenga chuki, hasira na uhasama kati ya wanajamii na ndugu wa marehemu kwa upande mmoja na Jeshi la Polisi kwa upande mwingine.

Katika matukio ya hivi karibuni, familia mbili zilisusa kuchukua maiti za wapendwa wao kutoka mochwari kwa ajili ya maziko wakidai uchunguzi huru na wa kina wa vifo wanavyovihusisha na polisi.

Mkoani Mbeya, ndugu wa marehemu Frank Kapange, wamesusa kuchukua mwili wake zaidi ya siku 93 sasa wakiomba mahakama itoe amri ya kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu kifo chake wanachodai kilisababishwa na polisi.

Frank alifariki dunia Juni 4 na mwili wake kuhifadhiwa mochwari katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Hukohuko Mbeya, Machi 25 wakazi wa Kata ya Iyela walizusha tafrani kubwa kufuatia kifo cha Allen Mapunda (22), aliyedaiwa kufariki dunia saa chache baada ya kuachiwa kutoka kituo kikuu cha polisi alikokuwa akishikiliwa.

Jijini Dar es Salaam, familia ya Kindamba iligoma kwa zaidi ya wiki mbili kuchukua mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba aliyedaiwa kupigwa risasi na polisi Agosti 11, kabla ya kuamua kumzika wiki iliyopita.

Vilevile, Agosti 29 polisi mkoani Tabora walituhumiwa kumuua mfanyabiashara ya nyama, Selemani Jumapili (22) kwa kipigo huku Septemba Mosi wilayani Mufindi mkoani Iringa polisi wakituhumiwa kumuua kwa risasi abiria aliyekuwa kwenye gari aina ya Isuzu Canter baada ya dereva kukaidi kusimama.

Mtazamo wa kisheria

Akizungumzia matukio hayo, mwanasheria wa siku nyingi nchini, Francis Stolla anasema Taifa limegubikwa na wimbi la vifo vyenye utata na ni vyema matumizi ya Sheria ya Vifo (Inquest Act) na ile inayounda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (Permanent Commission of Inquiry Act) yakaanza.

Anatoa mfano wa jinsi Serikali ilivyoitumia Sheria ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kumchunguza aliyewahi kuwa mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake waliotuhumiwa kuwaua wafanyabiashara madini na dereva teksi hadi ukweli kujulikana.

“Watu waelezwe haki zao wazijue, wanataka kujua hatima ya ndugu yao. Kwa hiyo Serikali ijifunze kujibu na si kukaa kimya ili jambo lisahaulike,” anasema Stolla aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). “Ifike mahali tuweke utamaduni watu waone Jeshi la Polisi ni sehemu ya kukimbilia kupata haki na amani na wasijengewe mtazamo kuwa ni la kuepuka.”

Sheria ya Uchunguzi wa Vifo

Sheria ya Uchunguzi wa Vifo vyenye Utata (Inquest Act, 1980) inampa mamlaka Jaji Kiongozi kuteua ofisa mchunguzi wa vifo visivyo vya kawaida (coroner), ambaye ana mamlaka ya kuamrisha jeshi, daktari na yeyote anayeweza kusaidia katika uchunguzi kufika kuhojiwa na kutoa ushahidi.

Mchunguzi anapogundua ukiukaji wa taratibu hupeleka matokeo ya alichogundua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).

Pale ambapo Jaji Kiongozi hachagui ofisa mchunguzi, hakimu yeyote wa wilaya au mkoa ama eneo husika atafanya kazi kama ofisa mchunguzi kuchunguza kifo chenye utata au mtu anayefia mikononi mwa polisi.

Jambo ambalo watu wengi hawafahamu ni kwamba mtu yeyote anayepatwa na masaibu ya kupoteza ndugu au jamaa katika mazingira yenye utata anaweza kupeleka maombi mahakamani ili kifo hicho kichunguzwe na ofisa uchunguzi.

Kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), tatizo la vifo vinavyotokea mikononi mwa vyombo vya dola au vinavyosababishwa na matumizi makubwa ya nguvu vinaongezeka miaka ya karibuni.

Kwa upande mwingine, Stolla anasema matukio ya watu kuumia ama kufia mikononi mwa polisi huanza pale utaratibu wa ukamataji wa watuhumiwa kwa mujibu wa sheria unapokiukwa.

Anasema mtuhumiwa yeyote ana haki nyingi mojawapo ikiwa ni ile ya kuchukuliwa hana hatia (presumption of innocence), kabla hatia yake haijathibitishwa na mahakama.

“Mtuhumiwa yeyote hapaswi kuchukuliwa hatua kwa kupigwa ama kuteswa hata kama ameonekana ameiba hadharani mpaka chombo cha kuthibitisha hatia yake kitakapoamua,” anasema Stolla.

Anasema, “hii haki ya kuchukuliwa hana hatia inavunjwa na wananchi wenyewe na vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi. Mtu anapokamatwa tayari wanamchukulia kama mkosaji. Utakuta mtu yuko chini ‘ame-surrender’ lakini bado wanampiga.”

Polisi wasijichunguze

Stolla anasema sasa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki ya mtu kupewa fursa ya kusikilizwa kabla ya kuadhibiwa. Haki hiyo, anasema, imekuwa ikikiukwa mara nyingi pale polisi wanapojitwika jukumu la kuchunguza mauaji wanayotuhumiwa.

“Kwa sheria ya asili kabisa, mtu au taasisi haitakiwi kufanya maamuzi katika shauri linalokuhusu ambalo ana masilahi nalo. Kama polisi ndiyo wanaotuhumiwa hawatakiwi kuhusika na uchunguzi, bali inatakiwa iundwe tume huru.”

Ripoti za haki za binadamu

Ripoti ya Haki za Binadamu ya LHRC ya mwaka 2014 hazionyeshi kuwepo matukio kama hayo kwenye rekodi za polisi.

Kituo hicho kinasema kilirekodi matukio takriban sita ya watu kufa kwa madai ya kipigo cha vyombo vya dola, matumizi ya nguvu yaliyopitiliza.

LHRC wanakiri kuwa kumekuwapo na ugumu wa kupata takwimu kuhusu idadi ya watu waliofikwa na madhila hayo Tanzania kwa polisi ama kutokuwa na takwimu hizo au kutokuwa tayari kuzitoa kwa umma.

Taarifa rasmi ambazo LHRC ilizipata kutoka polisi zinaonyesha kuwa mwaka 2015 hakukuwa kabisa tukio la namna hiyo nchini.

“Hii inaweza kumaanisha kuwa hali imeboreshwa kuhusiana na vyombo vya usimamizi wa sheria. Hata hivyo, uchunguzi huru unahitajika kuthibitisha kama hali hiyo ni halisi kwa sababu bado kuna malalamiko mengi ya vifo vinavyodaiwa kusababishwa na matumizi ya nguvu toka vyombo vya dola,” inasema taarifa hiyo.

Mwaka 2016, LHRC ilirekodi matukio manne ya mauaji yaliyosababishwa na vyombo vya dola wakati ripoti rasmi ya polisi inaonesha kulikuwa na tukio moja.

Matukio hayo yalionekana kushika kasi zaidi mwaka 2017 na hadi kufikia Juni, matukio tisa yalikuwa yamerekodiwa ikiwa ni ongezeko la matukio matano zaidi kulinganisha na mwaka 2016.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga anasema tatizo kubwa la matukio kama hayo kuendelea kuwapo ni pale wanaotuhumiwa kuua ndiyo wanajipa mamlaka ya kuchunguza.

“Kesi ya nyani huwezi kupeleka kwa ngedere,” anasisitiza.

Anasema LHRC ilipendekeza wakati wa kutoa maoni ya Katiba mpya kuwepo na chombo huru cha kusimamia mwenendo wa Jeshi la Polisi, ambapo matukio kama hayo yanaweza kupelekwa na kuamuliwa kama ilivyo nchi nyingine.

Lugola asisitiza uthibitisho

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola anasema bado hajapokea ripoti ya uchunguzi wa matukio ya namna hiyo ambayo imethibitisha kuwa mtu amekufa kwa kipigo cha polisi.

“Ukweli wa mambo haya una uhusiano na majibu ya postmoterm (uchunguzi wa kitabibu wa sababu ya kifo), mimi sijapata tukio la mtu alikufa kituoni na ikathibitisha tumegundua alipigwa na polisi,” alisema Lugola wiki iliyopita.

“Kwa hiyo hili suala ni gumu kulisemea wakati hakuna tukio lililothibitishwa na uchunguzi.”

Alipoulizwa ni kwa nini sheria ya vifo vyenye utata isitumike badala ya polisi wanaotuhumiwia kuunda timu ya uchunguzi, Lugola alisema: “Kila tukio likitokea lenyewe kwa nature (asili) yake litatuongoza cha kufanya. Si kila tukio linashughulikiwa sawa na lingine. Matukio hayafanani, kwa hiyo huwezi kuwa na fomula moja.”