Maiti iliyosuswa Mbeya bado kizungumkuti

Muktasari:

  • Frank alifariki dunia Juni 4 katika tukio ambalo liligubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini Mbeya, alifariki dunia kwa kipigo akiwa mikononi mwa Polisi, hivyo kususia mwili huo ambao hadi sasa upo chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ikiwa ni siku ya 91.

Mbeya. Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya umesema umeshindwa kutekeleza amri ya kuutoa kwa ndugu ama kuuzika mwili wa Frank Kapange (21) kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kutokana na kupokea hati ya rufaa kutaka kutotelekeza amri hiyo kwa vile kesi hiyo imepelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Frank alifariki dunia Juni 4 katika tukio ambalo liligubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini Mbeya, alifariki dunia kwa kipigo akiwa mikononi mwa Polisi, hivyo kususia mwili huo ambao hadi sasa upo chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ikiwa ni siku ya 91.

Baada ya familia hiyo kususia mwili huo, waliamua kufungua shauri Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya wakiiomba kutoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina juu ya sababu za kifo cha kijana wao.

Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank kuchukuliwa na ndugu ili ukazikwe baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ikisema imeridhishwa na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawikili wa upande wa Serikali.

Pia, Mteite alitoa amri kwa mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, kuutoa mwili huo na kuukabidhi kwa ndugu ili wakauzike kama ilivyo utamaduni wa Afrika badala ya kuendelea kuuacha chumba cha maiti muda wote huo na kwamba endapo ndugu hao watagoma, uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na kitengo cha afya cha Jiji la Mbeya ufanye utaratibu wa kwenda kuuzika.

Msimamo wa hospitali

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Godlove Mbwanji alisema awali, alipokea maelezo ya hukumu hiyo ya kuutoa mwili wa Frank kwa ndugu zake ili taratibu za maziko zifanyike na kama hawatafanya hivyo, hospitali yake kwa kushirikiana na kitengo cha afya cha Jiji la Mbeya wabebe jukumu la kuuzika mwili huo.

Hata hivyo, alisema kabla ya kutekeleza amri hiyo, walipokea hati ya rufaa kutoka kwa wakili wa familia ya Kapange inayoonyesha wamekata rufaa juu ya amri hiyo, hivyo kusitisha mchakato wa kutekeleza amri hiyo hadi uamuzi wa rufaa hiyo utakapotolewa.

“Nimepokea ile hukumu ikitutaka kutekeleza amri, lakini pia tukataletewa hati ya rufaa kutoka kwa ndugu ikionyesha kuna rufaa mahakamani kuhusiana na suala hili. Hivyo hatuwezi kutekeleza amri hiyo wakati imefutwa na rufaa hii.

Sasa tunasubiri uamuzi mwingine kulingana na rufaa hiyo. Tunaendelea kuuhifadhi mwili wa marehemu huyo,” alisema Dk Mbwanji.