Diamond afungua njia Afrika Magharibi...

Saturday December 14 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kiwanda cha muziki wa kizazi kipya maarufu Bongofleva kina mashabiki na wasanii wengi pengine ikishindana kwa karibu na wapenzi wa mpira wa miguu.

Wengi zaidi kwenye kiwanda hiki ni vijana, wapo waasisi, waliojiunga kati kati na wanaochipukia. Miongoni mwao kuna wasanii waliojiunga na kiwanda hicho kikiwa kimeshaanza lakini wanafanya vizuri wakisonga mbele na baadhi ya wakongwe wakirudi nyuma na wengine kukimbia kabisa.

Miongoni mwa wasanii walioikuta Bongofleva na kuendelea hadi kuota mizizi kwenye fani hiyo huku akiwa juu ni nyota wa wimbo ‘Baba Lao’, Diamond Platnumz, ambaye mwaka huu ametimiza miaka 10.

Platnumz ametimiza miaka 10 kwenye kiwanda cha burudani akiwa kwenye ubora wake , huku kila kukicha akipasua anga.

Nyota huyo wa albamu ya ‘A Boy From Tandale’ ameshirikiana na wasanii kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika, kiasi cha kuipeperusha bendera ya Bongofleva kwenye kila kona ya mipaka ya nchi.

Albamu ya A Boy From Tandale ilizinduliwa rasmi Machi 14, 2018 Nairobi nchini Kenya ambapo wasanii wote kutoka WCB walishiriki pamoja na staa kutokea Marekani, Omario ambaye pia ameshiriki kwenye wimbo wake unaokwenda kwa jina la ‘African Beauty’.

Advertisement

Wasanii kutoka nje ya Tanzania walioshiriki kwenye albamu hiyo yenye nyimbo 18 ni kundi la Morgan Heritage (Jamaica), Jah Prayzah (Zimbabwe), Omario, Rick Ross na Ne-Yo (wote Marekani), pia kuna Tiwa Savage, Davido, P Square na Mr. Flavour hawa wote kutokea Nigeria.

Katika kuhakikisha anawafikia wapenda burudani popote pale walipo, staa huyo amepeleka burudani nchini Sierra Leone ambako amekusanya kijiji kama ambavyo amekuwa akifanya kila nchi anapokwenda kufanya shoo.

Licha ya kutumbuiza katika tamasha linalojulikana kwa jina la Ecofest, lililojumuisha wasanii wengine kutoka nchini humo, mashabiki walionekana wazi kuhitaji huduma ya baba huyo wa watoto watatu kutoka nchini Tanzania.

Waziri Ally ‘Njenje’ ataja fursa za Afrika Magharibi

Inawezekana ukajiuliza kwa nini Diamond ameibuka Afrika Magharibi. Mwanamuziki mkongwe nchini Waziri Ally ambaye ni kiongozi wa Bendi ya Kilimanjaro, ‘Wana Njenje anasema Diamond anakwenda Afrika Magharibi kwa sababu walitangulia miaka mingi na muziki wao ulishakubalika duniani.

Anasema kuwa yeye anapata nafasi ya kujisogeza kupata ushauri mpya, wafadhili na masponsa wapya ambao wana uzoefu wa kuwauza au kuwatangaza wanamuziki kimataifa zaidi.

Pia lazima atapata promosheni, wale masponsa na mapromota wanafanya biashara kazi yao ni kuwasogeza wasanii kwenye fursa

“Wanaangalia hapa ninaweza kufanya biashara, hivyo wanaingia naye mkataba wa muda mfupi hata wa mwezi mmoja au wa muda mrefu, ”anasema Waziri Ally ambaye alianza muziki katika kundi la Lucky Star miaka ya 60.

Anasema Diamond anakwenda nje lakini kuna kona fulani ukiweza kuzipenya ambako wamefikishwa kina Salif Keita maarufu “Golden Voice of Africa”, Mamadou Diabaté.

“Kutokana na mchanganyiko huo itakuwa rahisi kwa Diamond kupasua anga zaidi, kwa sababu wasanii kutoka Afrika Magharibi wengi walifanikiwa kuupeleka muziki wao kimataifa.

“Simaanishi muziki wa kijana huyo haujafika kimataifa, ninachosema kwa njia hiyo utajikita na atapata dili nyingi zaidi, inawezekana ana sababu nyingine lakini kwa mtizamo wangu hili ndilo lengo lake hasa,” anasema.

Kuhusu aina ya muziki Ally ambaye mwaka 1978 alijiunga na bendi ya Msondo, anasema mbali na Afro Bongo ambayo Diamond anapiga kwa sasa anasema hakuna ubaya kama watakuwa wanafananisha muziki wa ndani na wa sehemu nyingine badala ya kuiga.

Anasema pamoja na vijana kufanya vizuri na kuwa na mashabiki kuna changamoto anaziona, ambapo msanii akifanya kitu chake cha hapa nyumbani ambacho hakuiga, walaji hawakikubali.

“Zamani tulianza kuiga muziki wa Kusini mwa Afrika, Congo na sasa Magharibi mwa Afrika, sasa msanii asipoiga hapokelewi kwa muziki wake mwenyewe.

“Changamoto nyingine ni watayarishaji wanaowatengenezea muziki vijana mara nyingi na wao wana tabia ya kuchukua vionjo vya muziki wa Afrika Magharibi, tukidhani kwa sababu wamekubalika duniani nasi tutakubalika kumbe si kweli,” anasema Waziri Ally.

Anasema kwa kiasi fulani Diamond anakutana na hili anapofanya kolabo na wanamuziki wa nje wenye majina makubwa kwa lengo la kuvutia mashabiki wa msanii huyo, jambo ambalo linawavutia masponsa wake na mapromota.

“Bongofleva ni muziki mkubwa sana na siyo kwamba lazima uchanganye na vionjo vya nje, tumefanya wimbo na Kassim Mganga ‘Somo’, MwanaFA ‘Kama zamani, ” anasema.

Kuhusu wasanii wa miondoko ya Bongofleva kutopiga laivu mwasisi huyo wa Tamasha la Sauti za Busara anasema wasanii wanatakiwa kulifanyia kazi suala hilo.

Anasema akiwa miongoni mwa waanzilishi wa Tamasha la Sauti za Busara akishirikiana na baadhi ya watu akiwamo marehemu Ruge Mutahaba, Marehemu Yusuph Chuchu, Ahmed Juma na Simai Mohamed Said ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, aliwahi kutoa rai kuwa washiriki wote wa tamasha hilo lazima wapige laivu.

“Nilitishiwa kwa kweli na baadhi ya wasanii, wakiona kama ninawanyima fursa, lakini nikiwa Makamu Mwenyeki sikuwahi kulikubali hilo,” anasema mkali huyo wa kupiga kinanda.

Anasema cha kushangaza huko wasanii wa Tanzania wanakoiga muziki Afrika Magharibi, wao huja na vifaa vyao vya asili kwenye tamasha hilo, wanapiga Hip Hop yenye vionjo vya asili wakiwa na makora yao, dramz zao na hawapigi play back wanapiga laivu.

“Nimefanya kila kitu kama Njenje hadi semina wakati vijana ndiyo wanaibukia hususani Hip Hop wakatubishia, hili ni tatizo kwenye tasnia yetu hususani vijana wanaopenda kurahisisha.

“Wengi wanamtegemea mtu mmoja ambaye ni prodyuza, ana wasanii 10 kama wewe na yeye ana nyimbo zake mbili, halafu unategemea atatayarisha muziki mzuri,” anasema.

Anafafanua kuwa si rahisi kuwa na kichwa cha aina hiyo kinachoweza kutofautisha muziki wa huyu na wa huyu ikiwamo wa kwake, matokeo yake nyimbo zote zinafanana huku vionjo vya biti vikiwa vya kuiga.

Alichofanya Diamond ni kama kufungua njia huenda siku zijazo muziki wa Bongo ukatamba Afrika Magharibi.

Advertisement