KITABU CHA WIKI: Fikra hasi ndiyo adui yako

Je, imekwishakutokea ukajiona kama huna thamani yoyote hapa duniani au kuhisi kama watu wote wanaokuzunguka wanakuona wewe si muhimu?

Hali hii ya kuwa na mawazo yenye fikra hasi imekuwa ikiwakumba watu wengi duniani kiasi cha kuharibu kabisa mipango yao katika maisha.

Mwandishi Ryan Holiday ameandika kitabu na kutoa ufumbuzi. Kinaitwa ‘Ego is the enemy. Ni matunda ya utafiti wake mwingi kuhusu namna binadamu anavyojifikiria na kujitathmini, hali inayoweza kumfanya apate matokeo ya aina fulani katika kipindi cha maisha yake.

Kitabu hiki kinatoa suluhisho la jinsi ya kujithamini, kufikiri na kuweza kuziondoa zile fikra hasi tunazokuwa nazo muda mwingi katika maisha yetu ya kila siku.

Kimeelezea jinsi mtu anavyojiona kwa nje na kwa ndani na jinsi matokeo yake yanavyokua. Kinazungumzia ile hali ya kutojiamini, kujisikia huwezi kufanya kitu fulani na pia kujiona kama wewe si wa muhimu katika jamii inayokuzunguka.

Mara nyingi watu wengi tumekuwa tukijiangalia katika fikra hasi, lakini ni wajibu wetu kujitathmini na kujiangalia na kujitafakari kila mara ili kuweza kujiimarisha.

Kitabu hiki kimegawanyika katka sehemu kuu tatu ambazo zinaonyesha uhalisia wa maisha yetu, Mwandishi kaelezea nyakati za kuwa na hali ile ya kujiwekea fikra hasi, pia kuvutika na kuwa na hamu ya kufanikisha lengo kubwa na zuri, kupata mafanikio na kupongezwa na jamii na pia kushindwa yaani kuanguka na kufanyia kazi kile kitu kinachokufanya uanguke.

Mwandishi anatoa mafunzo ya maana na yenye tija ambayo tunayaweza kuyatumia mara tunapojikuta tukiwa katika hali hizo katika maisha yetu. Ameelezea jinsi ya kufikiria kuhusu malengo yetu, jinsi ya kuwa na uhusiano mzuri na wenzetu na sisi wenyewe binafsi, jinsi ya kuwa watu wa kawaida bila kuwa na majivuno, jinsi ya kutatua changamoto zinazotukabili au kuanguka katika kitu chochote kile.

“Uwezo wa kujitambua, kujitathmini uwezo wako ni kitu muhimu sana, bila kufanya hivyo ni ngumu sana kujiimarisha na inasababisha kupata shida ya kusonga mbele” anasema Holiday. Anashauri namna ya kufanyia kazi yale mabaya ambayo tumekuwa tukijiwazia ili tuyabadilishe.