Kama miezi ingekuwa ni watu; mwezi Januari ungekuwa nani?

Ulishawahi kuufikiria mwezi wa Desemba na Januari, ukajiuliza hii miezi ingekuwa binadamu ingependeza kuwa nani?

Mzazi, Mwalimu, Rafiki, Ndugu, Jirani? Na vyovyote ambavyo ingekuwa ingependeza kuwa ya aina gani?

Yaani kama mzazi ingependeza kuwa mkali, mpole, anayefuatilia sana, au asiyejali kabisa?

Vipi Desemba ingekuwa Rafiki tena mwanafunzi wa chuo ambaye mmekutana chuoni. Halafu anajua una pesa kwa ajili ya kulipia ada ya muhula mzima ujao; hapa pesa ni mshahara wako wa Desemba na muhula mzima ujao ni mwezi Januari, si unajua mwezi wa kwanza ni mchanganyiko wa miezi sita kwa wakati mmoja ni kama muhula mzima tu.

Halafu sasa Desemba ni mwanafunzi ambaye anaelewa kwamba jukumu kubwa la uhai ni kufurahia maisha. Kwake ni heri kufa na miaka 23 ukiwa umefurahia maisha kwa kufanya starehe kuliko kufa na miaka 76 ukiwa umeishi maisha yaliyopooza.

Sasa anakutambulisha kwenye ulimwengu wake. Anafanya juu chini kuhakikisha unaamini kwamba, maisha uliyokuwa unaishi Novemba na miezi mingine nyuma yale si maisha, kule ni kuwa hai tu. Maisha ni haya ya kwake.

Hapo ndiyo maana Desemba ana kila namna ya sikukuu na likizo. Na sababu nyingi za kukuongezea matumizi ambazo unaweza usizione hadi mwezi ukipita.

Ukiamka asubuhi, ukitaka kunywa chai ya kawaida, anakwambia hapana, wewe si una pesa ya ada, kwanini usichukue kidogo ukagonga chai nzito, halafu jioni tukachukua uber/taksi, tukaenda sehemu, tukanywa, tukachoma nyama halafu tukitoka, utamtafuta mjomba yako akupe pesa ya ada.

Hapa ndiyo unajiona Desemba unakuwa na aina ya matumizi ambayo hata huelewi kwanini unatumia hivyo, halafu ukiwa na imani ya kwamba, pesa ikiisha, ambayo ni mshahara, kuna sehemu utaenda kukopa mkopo unaoufikiria ndiyo mjomba. Na kweli unafanya kama unavyoshauriwa na Desemba unakula maisha.

Januari yeye anapendeza kuwa mzazi ambaye ukikosea wala hakuadhibu, anaacha kosa lako likutafune ndani kwa ndani yeye akikuangalia tu bila msaada wowote. Yaani kama umekula ada, ambayo ndiyo kumaliza mshahara wa Desemba, na umefukuzwa chuo, ambayo ndiyo kumaliza mwezi Desemba, na ikabidi urudi nyumbani kwa mzazi wako, ambayo ndiyo kuingia mwezi Januari. Yeye Januari hakukugusi, anaacha kosa lako likuadhibu, yaani badala ya kula zile nyama choma na kunywa sana, unarudi kwenye maisha yako ya Novemba na miezi ya nyuma, tena ubaya ni kwamba hali yako inakuwa mbaya zaidi.

Hapa ndiyo unakuta mtu anaishi maisha kama rejeta. Kifungua kinywa ni maji, chakula cha mchana ni maji na usiku pia maji. Sio kwa kupenda, ni nguvu na miujiza ya Januari.