SIMULIZI ZA MUZIKI: Kiingilio bia si dhana mpya katika muziki wa bendi

Nimepigiwa simu na mwanamuziki mmoja rafiki yangu akilalamika kuwa ni wiki ya pili sasa bendi yake haijapiga muziki kwa sababu baa ambazo walikuwa wanapiga zimeamua kupunguza malipo kutokana na kupungua wateja. Mambo mengi yamenijia kichwani niliposikia hili, nimekumbuka utamaduni wa kupiga muziki kwenye mabaa bila kiingilio ulipoota mizizi.

Utamaduni wa bendi kupiga madansi na kulipwa kwa kuburudisha wanywaji si jambo geni duniani, hapa Tanzania jambo hili lilipata msukumo zaidi mwishoni mwa miaka ya 90 wakati kulikuwa na ushindani mkubwa wa kampuni kubwa mbili za kutengeneza bia. Moja ya kampuni hizi ilianza kutumia mbinu ya kukodi wasanii na kuwazungusha katika baa mbalimbali kufanya maonyesho ya kuhamasisha mauzo ya vinywaji vyake, utaratibu uliopewa jina la ‘promosheni’, awali walikuwa wakikodishwa wasanii wachekeshaji, wacheza sarakasi, ngoma na kadhalika, baadaye zikaanza kuhusishwa bendi mbalimbali za muziki. Kutokana na ushindani wa kibiashara, moja kati ya kampuni hizi ilipotea kwenye soko, upinzani wa kibiashara ukawa umepungua hivyo hata ile kampuni iliyobaki taratibu ikajiondoa katika shughuli za kukodi wasanii na kuwazungusha kwenye baa mbalimbali.

Lakini kufikia wakati huo utamaduni wa kutumia bendi za muziki kuita wateja kwenye baa ulikuwa umeshaota mizizi, na kuanzia wakati huo bendi nyingi zimekuwa zikifanya kazi katika mazingira hayo ya kutegemea kupiga muziki katika baa ili kupata kipato chao.

Kama nilivyosema kuwa mtindo wa kupiga kwa ajili ya kuburudisha wateja si mgeni duniani ila kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa sasa hapa nchini na sehemu nyingine.

Pengine hii ni kutokana na jinsi mfumo huu ulivyoanza, kwani haukuanzishwa na wanamuziki bali kampuni za kuuza pombe. Miaka ya nyuma hoteli nyingi zilizokuwa chini ya Bodi ya Utalii nchini zilikuwa na bendi zilizoitwa ‘ resident band’ kimsingi hakuna tofauti ya malengo ya bendi hizi na zinazopiga kwenye baa siku hizi. Bendi maarufu kama Bar Keys, ambayo sasa inafahamika kama Tanzanites, The Revolutions inayojulikana kama Kilimanjaro Band zilifikia mpaka kupewa vyumba vya kulala wanamuziki katika hoteli hizo na hata kupewa chakula cha siku nzima, kazi kubwa ya bendi hizi ilikuwa ni kupiga muziki wa kuvutia wateja kwenye hoteli hizi.

Tofauti na ilivyo sasa bendi hizi zilikuwa na mikataba ya malipo. Hivyo basi ikinyesha mvua au likiwaka jua, bendi hizi za hotelini zilikuwa zikilipwa kiasi ambacho kilikubalika katika mikataba. Malipo hayakutegemea kuyumba kwa biashara ya hoteli.

Katika nchi nyingine kampuni za bia ndizo huwa zinaingia mikataba moja kwa moja na bendi katika kufanya maonyesho ambayo yatasaidia katika kutangaza bidhaa zao, katika mfumo huo wanamuziki huwa wanapata kipato kizuri tofauti na mfumo uliopo wa kulipwa na wafanyabiashara wa rejareja wa vinywaji.

Kupiga kwenye baa katika nchi nyingine huwa ni kwa bendi ndogo ambazo zinatafuta ‘kutoka’. Bendi ndogo hutumia maonyesho haya kwenye baa kujijenga na kutengeneza staili zao na kisha kurekodi nyimbo zao ili kujiwekea nafasi katika ushindani mkubwa uliopo katika ulimwengu wa muziki. Hali ni tofauti na hapa kwetu kwa kuwa huku hata bendi ‘kubwa’ nazo zinapiga muziki wa kiingilio bia.

Mwaka 2000 baadhi ya wanamuziki walijikusanya kujaribu kuunda chombo kilichoitwa Union of Tanzanian Musicians (Utamu). Nia ya chombo hiki ilikuwa ni kupata muungano ambao utaangalia maslahi ya mwanamuziki kama mfanya kazi. Utamu haikufika mbali kwani kwanza wanamuziki wenyewe hawakuiunga mkono labda kutokana na kutofahamu umuhimu wa chombo hicho katika maslahi yao, pili chama kilichokuwa cha wafanyakazi wa majumbani na mahotelini, kilijitokeza na kudai kuwa wanamuziki ni kati ya wafanyakazi walioorodheshwa katika kundi lake la wafanyakazi. Kukosekana kwa chama cha kulinda maslahi ya wafanyakazi wanamuziki, ni moja ya sababu ambazo zinayumbisha kipato cha wanamuziki hasa wa bendi, kwani hakuna viwango vyovyote vinavyofuatwa, na hivyo kuleta fujo katika tasnia. Wanamuziki wenyewe wamekuwa wanalalamikiana kuhusu tabia za wenzao ambao hushusha bei za kukodishwa mpaka kufikia kiwango ambacho ni cha chini mno. Si ajabu kusikia bendi yenye watu saba ikakodishwa kupiga muziki kwa masaa sita ikakubali kulipwa Sh 150,000. Kwa hesabu hiyo hujui hata hawa wanamuziki wanagawana vipi pato lao baada ya kulipia gharama za kukodi na kuvisafirisha vyombo na usafiri wao.

Mwisho ni woga wa wanamuziki ambao hawajawahi kupiga muziki wa kiingilio, wengi huwa hawana imani kuwa watu wanaweza kuingia kwa kulipia. Kitendo hiki cha baa kuamua kushusha viwango vya malipo, wakati huwa haviongezi siku vikipata faidi ni nafasi nzuri ya Bendi ‘kubwa’ kujitathmini kuhusu suala la kuendelea kuishi kwa kutegemea malipo kwenye baa. 2020 ifungue ukurasa mpya.