Miaka 15 ya maisha bila ya figo moja

Wakati mwingine katika maisha uvumilivu ni kitu kinachotakiwa kukutawala ili ushinde kila jaribu au njia ngumu unayokutana nayo.

Uvumulivu huo umethibitika kwa Asia Mustapha ambaye ameishi bila figo kwa miaka 15 sasa, lakini uso wake umejaa tabasamu, matumaini na subira jambo ambalo huweka ugumu kwa mtu asiyemfahamu kujua tatizo lake.

Gazeti la Mwananchi limefanya naye mahojiano kwa kina ili kujua ni namna gani ameweza kukabiliana na tatizo hilo kwa muda mrefu.

Mwandishi: Tueleze historia yako kwa ufupi?

Asia: Asia ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili aliyezaliwa akiwa na afya kama wengine. Nimesoma Shule ya Msingi Diamond Olympio na nilipofika darasa la pili mwaka 1994 nilipata tatizo la kichwa lililokuwa likinisumbua mara kwa mara na kila nikipelekwa hospitali halionekani.

Nikawa naendelea na maisha ya kumeza panado (dawa ya kutuliza maumivu) hadi nilipomaliza darasa la saba na kujiunga na Shule ya Sekondari Cambridge iliyopo jijini Dar es Salaam. Lakini kutokana na kuugua mara kwa mara ilibidi nihamishiwe Shaban Robert na kurudia tena kidato cha kwanza mwaka 2002 nilikosoma hadi kidato cha tatu baada ya tatizo hili kugundulika.

Mwandishi: Uligunduaje kama una tatizo la figo?

Asia: Haikuwa rahisi kugundua kama nina tatizo hili. Nilipokuwa kidato cha tatu nilikuwa nikipata tatizo la kuvimba kwenye mdomo kwa juu na macho. Nilikuwa napelekwa hospitali na kupewa dawa za mzio. Nikimaliza tatizo linaonekana kuisha lakini baadaye linarudi.

Baada ya kuonekana tatizo hili linajirudia mara kwa mara, baba aliamua nipime vipimo vyote, kama moyo na tulipewa siku za kufuata majibu ndipo ilipogundulika kuwa figo zangu haziwezi kufanya kazi tena na hiyo ilikuwa mwaka 2004.

Mwandishi: Baada ya kugundulika na tatizo hilo, ilikuwaje?

Asia: Baada ya kugundilika figo zangu hazina uwezo wa kuchuja uchafu ilinilazimu nianze kusafishwa damu na nilikuwa nikifanya hivyo mara tatu kwa wiki. Mwaka 2005 nilipata ndugu yangu ambaye alinipatia figo yake moja na nashukuru Mungu niliendelea vizuri na nilikaa nayo kwa miaka sita.

Lakini kabla ya kufanya upandikizaji wa figo mwaka 2005 nchini India, nilipata shida ya moyo nikapewa dawa ambayo baada ya kutumia iliniharibu masikio na kunifanya kuwa kiziwi kabisa.

Nilipoenda kufanyiwa upasuaji wa figo daktari aliniambia hauwezi kwenda sambamba na upasuaji wa masikio kutokana na dawa za usingizi zinazotumika, hivyo inabidi nisubiri kwa miaka miwili. Mwaka 2008 nilirudi India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa masikio. Nilifanikiwa kutokana na kuwekewa vifaa vya usikivu lakini nilishindwa kuendelea na shule kwa sababu daktari alisema kutokana na kukaa muda mrefu bila kusikia inabidi nisubiri ubongo uchangamke ndiyo nirudi shule.

Mwandishi: Kwanini haukurudi shule tena baada ya kupona masikio?

Asia: Baada ya kukaa nyumbani na akili kuchangamka mwaka 2011 figo niliyokuwa nimepewa na ndugu yangu iliharibika hivyo ilinibidi tena kwenda India.

Rafiki yangu mwingine alinipatia figo yake lakini ilishindikana kutokana na maambukizi katika damu niliyokuwa nayo. Tangu 2011 nilianza kuishi maisha ya kusafisha damu na mpaka sasa sina figo naishi kwa msaada wa mashine inaitwa ‘dialysis machine’ niliyowekewa kifuani kwangu.

Mashine hiyo hutumika kwa ajili ya kusafisha damu na ninapokwenda hospitali huunganishwa na mipira maalumu huku kwenye mashine kukiwa na figo bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na kuirudisha mwilini na hufanya hivyo angalau mara tatu kwa wiki.

Mwandishi: Sasa hivi unajishughulisha na nini?

Asia: Nimeajiriwa Global Publishers, lakini kutokana na kuumwa mara miguu, mgongo, kiuno nimeacha kwenda kwa kuwa wakati mwingine nimekuwa nikishindwa hata kunyanyua mguu kuingia katika daladala.

Mwandishi: Wazo la kuandika kitabu lilitoka wapi?

Asia:Kutokana na yale niliyopitia katika maisha yangu nilitaka kuwapa moyo watu wengine wanaopitia hali kama yangu kwa njia ya maandishi. Katika kitabu hicho nimeongelea mambo mengi, hasa suala la lishe za wagonjwa na namna ya kutunza figo.

Pia, niliandika kitabu hiki ili kutafuta pesa za kufanyiwa upandikizaji wa figo nyingine. Nilitarajia mauzo ya kitabu hiki ndiyo yatumike kwenda kupandikiza figo, jambo ambalo limekuwa kinyume.

Watanzania hawana desturi ya kupenda kujisomea na katika barua tuliyopewa inaonyesha kuwa matibabu ni dola 20,000 za Kimarekani zinahitajika (takriban Sh40.4 milioni).

Mwandishi: Je una furaha katika maisha yako?

Asia: Kuumwa si tatizo, maisha yangu yanaendelea japo sina figo nafanya kila kitu changu si wa kubebwa wala si wakuhitaji msaada wa karibu. Na hivi sasa nimekuwa mhamasishaji kwa watu walio na tatizo hili, kuwatia moyo na kuwapa mbinu za kufanya.

Nimekuwa nikiongea na watu mbalimbali wanaohudumia ndugu zao, wagonjwa wenyewe na ninawatia moyo ili waweze kupambana na ugonjwa huu huku nikiwaaminisha kuwa kuumwa si tatizo.

Kufuata masharti kama unayopewa baada ya kufanyiwa upandikizaji utaishi vizuri pamoja na kujaribu kujiepusha na msongamano katika kipindi cha awali, kuvaa mask, uangalie usafi wako kwa ujumla, kuangalia mazingira unayotumia ni moja ya vitu vya kuzingatia ili usipate maabukizi mengine.

Mwandishi: Kuna tofauti gani kati ya sasa na zamani?

Asia: Lazima tofauti itakuwapo maana tayari mwili umepungukiwa na viungo ambavyo hufanya kazi muhimu ya kuchuja taka katika mwili. Kwa kuwa tatizo langu nimelikubali na nimeona si tatizo, nahisi hicho ndio kinanipa nguvu ya kuendelea kupambana. Tofauti na hapo maisha yangu ni ya kawaida sana, japo wakati mwingine unakutana na maumivu kidogo lakini muda mwingi uko sawa na hii ni ushahidi kuwa inawezekana kuishi bila figo kama ukikubaliana na hali hiyo.

Mwandishi: Una chochote cha kuiambia jamii kuhusu ugonjwa wa figo?

Asia:Hili tatizo ni kubwa na linazidi kuongezeka kila kukicha, inabidi tupambane ili tuendelee kulitokomeza lisiendelee kuwaumiza wengine. Ni muhimu kila mtu anapojihisi hayupo vizuri apate ushauri wa daktari lakini si kununua dawa na kunywa kwa sababu wakati mwingine kufanya hivyo kunasababisha kujiumiza bila kujua.

Kama umeguswa kumchangia Asia katika matibabu unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0656 684 431