Unahitaji hatua za kisheria dhidi ya mdaiwa sugu

Mdaiwa mara zote huwa hataki kutimiza wajibu wake kama mlivyokubaliana kwenye mkataba wa mkopo. Hata lugha yake hubadilika tofauti na ile nzuri alivyokuwa nayo wakati anakopa.

Wakopaji wasumbufu wako wa aina mbili. Kwanza ni wale ambao wanawasiliana nawe na kuendelea kukupa ahadi ya kukulipa. Ni watu wa ahadi zisizotekelezeka.

Aina ya pili ni yule ambaye mnawasiliana, kuonana na kuongea anapohitaji mkopo tu, akishapata haumwoni tena. Akipigiwa simu hapokei. Hubadilisha njia na anaweza hata kuhama anapoishi.

Usipofahamu ni hatua unazopaswa kuchukua dhidi ya mkopaji msumbufu unaweza kupata hasara kubwa ambayo hukuitarajia. Mkopaji huyu anaweza kutumia kumfanya asilipe deni au umlipe fidia.

Kwa kutambua uwepo wa wakopaji wasumbufu ndio maana unashauriwa kuchukua tahadhari mapema kabla hujamkopesha mtu yeyote kwa kufahamu mambo ya msingi yanayomuhusu ikiwamo mikataba, anwani, mawasiliano, makazi, biashara au shughuli anayofanya.

Umuhimu wa taarifa hizi utauona atakapoanza kuwa msumbufu kwani zitakusaidia kufahamu hatua za kuchukua.

Jihadhari kuanzisha vurugu, lugha za matusi, uharibifu wa mali au chochote kilicho kinyume na sheria na usichukue sheria mkononi kwani itakugharimu.

Jambo la msingi ni kumpata kumdeni wako na kumsikiliza. Kumbuka, unao wajibu wa kutunza heshima ya mkopaji wako.

Baada ya kumtaarifu unaweza kuwajulisha wadhamini wake na kuwaeleza muda uliotoa wa mkopaji kulipa fedha anazodaiwa na hatua ulizopanga kuchukua endapo fedha hizo hazitalipwa ndani ya muda ulioutoa.

Taarifa kwa mkopaji ni muhimu zikatolewa kwa njia ya barua au notisi ya madai ambayo inaweza kuandikwa na wewe mwenyewe au wakili ili kuleta uzito wa madai yako.

Unaweza kumkabidhi jukumu la kudai deni lako dalali wa mahakama endapo kumtumia dalali hakutozaa matunda, fungua kesi mahakamani. Unaweza kuiomba mahakama imfunge mdaiwa kama atashindwa kulipa deni lako.