‘Wazee waendelea kuongezeka duniani kuliko watoto’

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018 imeonyesha kwa mara ya kwanza katika historia, kuna wazee wengi duniani kuliko watoto.

Takwimu zinaonyesha kuwa watu wenye umri wa miaka 65 ni wengi ukilinganisha na wale walio chini ya miaka mitano mwishoni mwa mwaka 2018

Kwa sasa kuna watu takriban milioni 705 wenye miaka zaidi ya 65 duniani, wakati wa wenye umri kati ya miaka 0-4 ni takriban milioni 680.

Christopher Murray, Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti na tathimini ya masuala ya afya ya Chuo Kikuu cha Washington ameiambia BBC : ‘’Kutakua na watoto wachache sana na watu wengi sana walio na umri wa miaka zaidi ya 65, hali itakayowia vigumu dunia kuendelea.

‘’Fikiria kuhusu athari za kisosholojia na kiuchumi kwa jamii yenye watu wenye umri mkubwa wengi kuliko watoto,’’ anaeleza.

Mwaka 1960, uwiano wa uzao ulikua karibu watoto watano kwa mwanamke mmoja, kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Karibu miaka 60 baadaye uwiano huo umeongezeka kwa 2.4 tu.

Tatizo la uwepo wa wazee wengi ni kubwa katika nchi zilizoendelea. Kuna kasi ndogo ya kuzaliwa watoto kwa sababu kadhaa ikiwemo sababu za kiuchumi, Idadi vifo vya watoto ni ndogo, njia za kupanga uzazi zinapatikana kwa urahisi na kulea watoto ni gharama.

Katika nchi hizo, wanawake hupata watoto wakiwa na umri mkubwa, hivyo huwafanya kuwa na watoto wachache.

Nchi za Kiafrika ni miongoni mwa nchi ambazo ziko kwenye njia panda kuhusu masuala ya uzazi: Viwango vya uzazi viko juu na hakuna uwiano kati ya idadi ya watu na ubora, Niger ikiwa moja ya nchi hizo.

Hata hivyo, nchi hizohizo zina idadi kubwa ya vifo vya watoto, Niger ikiwa na vifo 85 vya watoto katika kila watoto 1000, idadi kubwa duniani.

Kuwa na idadi kubwa ya wazee kuna maana kuwa kuna nguvu kazi ndogo, ambapo kunaweza kusababisha kushuka kwa uchumi wa nchi.

Novemba mwaka jana, Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilitahadharisha kuwa uchumi wa Japan unaweza kushuka kiasi cha zaidi ya asilimia 25 katika kipindi cha miaka 40 ijayo kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wazee.