UCHAMBUZI: Ukalimani wa lugha fursa inayowasubiri vijana

Saturday November 10 2018

 

By Kalunde Jamal

Kumekuwa na ombwe la baadhi ya fani kuwa na wahitimu wengi ambao wanakumbana na changamoto ya ajira kwa sababu ya wengi kuwapo sokoni.

Licha ya kila Mtanzania kuwa na haki ya kufanya kazi, bado kuna watu hususani vijana wanachagua kazi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 22 na 23 ya mwaka 1977 inaeleza kuwa kila Mtanzania anayo haki ya kufanya kazi na kupata ujira.

Lakini katika uchumi wa soko huria serikali inawajibika kuchangia asilimia 2.7 ya ajira na asilimia 98.3 inayobakia hutolewa na sekta binafsi na nyinginezo ikiwamo isiyo rasmi.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi duniani, (ILO), zinaeleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanakabiliana na tatizo la kukosa kazi.

Licha ya kuwapo kwa tatizo la ajira, bado kuna changamoto kwa vijana kuzisaka zilipo au kujipambanua kuzitafuta kwa mtizamo chanya.

Nasema hivyo kwa sababu kuna ajira zinakosa watu, lakini kulingana na mitizamo yao, wanashindwa kuzikimbilia.

Vijana wamekuwa wakichagua kazi au fani za kusomea na kujikuta waking’ang’ana katika fani moja, ilihali kuna fani nyingine zinahitaji wataalamu.

Yapo masomo yanayosubiri wataalamu waingie kwenye ajira ikiwamo wakalimani wa lugha mbalimbali.

Mbali ya wataalamu wa lugha, pia kuna nafasi ya wazi ya ajira kwa wataalamu wa lugha ya alama ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwakosa.

Serikali imetaja uhaba wa wakalimani wa lugha ya alama kama chanzo cha kuwanyima haki wenye uziwi na hata katika vyombo vya ulinzi.

Akifungua mkutano wa kitaifa wa ushawishi na utetezi wa lugha ya alama ulioratibiwa na Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa aliweka bayana kuwa kuna uhaba wa wakalimani nchini.

Ikupa alibainisha kuwa asilimia 98 ya Watanzania hawajui lugha ya alama na asilimia mbili iliyopo hawapewi nafasi pana, kusikilizwa na kutoa mchango wao kwa weye mahitaji.

Kwa minajili hiyo kuna fursa ya kuwa mkalimani wa lugha ya alama na lugha nyingine kwa ujumla.

Inaelezwa kua hapa nchini wakalimani wa lugha za alama hawazidi 20, lakini vijana wachache wanaotaka kusoma fani hiyo.

Badala ya kujazana kwenye kozi za uhasibu, ugavi, ualimu ambako kuna uhaba wa ajira, kumbe zipo fursa za wazi kama hiyo na hakuna anayezifikiria kwa sababu ya kuchagua kazi.

Kila mwaka wahitimu wengi wanamaliza masomo yao na kujikuta wakikaa nyumbani kutokana na kukosa ajira.

Inakadiriwa kuwa kila mwaka wahitimu wapatao laki hadi milioni moja huingia kwenye soko la ajira, ambapo asilimia 14.3 kwa wanawake na asilimia 12.3 kwa wanaume.

Hawa huingia kila mwaka kwa miaka mitatu watakuwa wamefurika, hivyo kijana unapaswa kujiongeza na kuangalia ni masomo yapi ukisoma yana fursa za ajira kama nilivyosema hapo awali badala ya kung’ang’ania zenye changamoto na wahitimu wengine.

Fursa haiji kama mana kutoka mbinguni bali inatafutwa na muda wa kuchangamka kuzitafuta ni wa ujana.

Jiongeze kidogo kwenye ukalimani kuna fursa.

Advertisement