Ni sawa kuwa washindani lakini isivuke mipaka

Ushindani ni moja kati ya vichocheo vya mafanikio ya jambo lolote duniani. Uzuri, ushindani huu unawapa walaji kilicho bora zaidi kwa sababu kila mmoja anaboresha bidhaa au huduma yake ili kuwavutia watu.

Jaribu kufikiria kampuni za umeme zingekuwa kama zile za simu au vyakula. Yaani unakuwa na uwezo wa kujiunga na kujiondoa kadri uwezavyo kutokana na ubora wa huduma zake.

Ushindani huu hauishii katika bidhaa na huduma, hata katika tasnia ya burudani upo, tena huku ndiyo kichocheo muhimu cha kuinogesha. Duniani kote ushindani zikiwamo tambo ni sehemu muhimu ya vinogesho.

Upande wa tasnia ya burudani hususan hapa nchini mambo yamekuwa tofauti kidogo. Wasanii wanatafutiana vijisababu vya kupigana vijembe na hatimaye wanatofautiana, jambo ambalo si zuri.

Mifano ya uhasama wa Dudubaya na Mr Nice iliyowafikisha hatua ya kupigana ngumi ni moja ya kupigiwa mfano kuwa ushindani hautakiwi kufikia hatua hiyo.

Nchini Marekani uhasama wa 2Pac na Notorious BIG uliwaondolea uhai. Ni mfano mwingine wa ushindani mbaya ambao wasanii hawatakiwi kuufikia.

Kumeshuhudiwa wasanii hasa wa muziki nchini ambao ni maadui na wamefikia hatua kuwa hawawezi kufanya kazi kwenye jukwaa moja. Mimi naona umeondoka kuwa uhasimu wa kikazi mpaka wa maisha binafsi.

Tukiangalia kwa mfano nchi za nje kama vile Marekani, wasanii ni kweli wanapigana vijembe, lakini ni kwa nia ya kupata changamoto ili kukomaa zaidi na wala si kuvimbiana hadi mbele ya mashabiki.

Kipindi cha nyuma msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo maarufu Ommy Dimpoz walipishana maneno na msanii mwenzake, Naseeb Abdul anayefahamika na wengi kama Diamond Platnumz.

Katika kurushiana maneno walivuka mipaka kwa kutoleana lugha chafu ambazo ziliwagusa watu wengine pia.

Ushindani na vijembe vinakubalika, lakini visiwe vya kuwadhalilisha wenyewe, marafiki au ndugu zao. Malumbano yale hayakuwa na tija katika ukuaji wa tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini.

Diamond Platnumz pia amekuwa katika uhasama na mwenzake, Alikiba. Hali hii kati yao imejenga sintofahamu kwa mashabiki wao ingawa ilikuwa sehemu ya burudani.

Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa uhasama huo umekuwa chachu ya Bongo Fleva kwani kila upande ulisubiria kusikia mwingine katoa kazi gani nzuri kumzidi.

Mashabiki wamekuwa wakichuana kuwashindanisha na mara chache walionekana kurushiana vijembe vya hapa na pale.

Unapokuwa ushindani wa kikazi kama ilivyo kwao ni wenye afya. Vijembe vya hapa na pale vimewafanya kuwa wasanii wakubwa Afrika Mashariki na Afrika, wenye wafuasi wengi.

Ukimzungumzia vibaya Diamond ni wazi mashabiki wake watakujia juu kama nyuki. Akizindua bidhaa watainunua au akifanya tamasha watajazana kumuunga mkono, vivyo hivyo kwa Alikiba.

Kwa hatua nyingine, baadhi ya wasanii siyo waadilifu wala wastaarabu. Kuna wale ambao ukiwafuatilia kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii hawana maadili.

Tanzania ni jamii moja ambayo mbali na mambo mengine, inashirikiana vitu vingi ili kuleta maendeleo.

Ni wakati wasanii wakae wajitafakari kuhusiana na vitu wanavyokuwa wakivifanya. Wao ni kama taa kwenye giza nene. Wanafahamika, kazi zao na pengine maisha yao kwa ujumla.

Ni wajibu wa kila mmoja kumuogopa Mungu na hapa heshima itatawala na umoja utazingatiwa. Taarifa za makundi kuvunjika na kugeuka kuwa maadui zitakoma.

Msanii wa Bongo Fleva, Tonny Jefferson kutoka Mwanza, anasema wasanii kama vile AliKiba na Diamond kwa sasa wako kimataifa. Iwapo wakipatana, muziki wa Tanzania utazidi kupenya zaidi licha ya jitihada walizonazo kwa sasa za kuupeleka.

Naye msanii Genevieve, anasema wasanii wa kike wakae chini wajitafakari. Watambue kwamba wana wazazi, watoto, wajomba na kadhalika. Kila wanachokifanya kinakuwa kama kioo kwenye jamii.

Hata hivyo, viongozi wa dini nao wanasema wasanii wengi hawatambui wala kukumbuka uwepo wa Mungu. Asilimia kubwa ya wasanii utawakuta wamelala siku za ibada kama vile Ijumaa na wikendi nzima, kwa kisingizio kwamba walikuwa ‘wanapiga shoo’ wiki nzima.

Kujisahau au kupuuza maadili ya Mtanzania kumechangia sehemu kubwa kwa matukio yanayoonekana kwa sasa.

Ni bora wasanii waache tofauti zao ili waweze kufika mbali. Hakuna msanii awe wa kuimba au wa filamu anayetaka kufanya kazi nchini tu bali kuwa kimataifa. Hili litawezekana iwapo kutakuwepo na ushirikiano na kuacha uhasama.

0744205617