Bado siku 105 hukumu ya Stars, Fainali za U-17 Aprili Tanzania

Monday January 7 2019

 

Dakar, Senegal

Mwaka mpya wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, umeanza kwa kuumiza kichwa, kwani mwandaaji wa fainali za mwaka huu zitakazoshirikisha timu 24 bado kujulikana.

Hata hivyo, CAF imesema Jumatano keshokutwa itampata mwenyeji wake kuandaa fainali hizo baada ya Kamati ya Utendaji kukutana.

CAF tayari imetangaza kalenda ya matukio yake ikianza na mkakati wa kuyafanya mashindano hayo kwa mara ya kwanza katikati ya mwaka kuyafanikisha utaratibu unaoanza mwaka huu.

Pamoja na hayo, CAF inaweza kujichanganya na mashindano yake kwani wakati ikihangaika na Fainali za Afcon 2019, kuna mashindano ya Vijana, mechi za klabu Afrika na mashindano ya soka kwa wanawake.

Kalenda ya CAF 2019 inaanza na Tuzo.

JANUARI 8

CAF itaanza mwaka wake kesho kwa kutoa tuzo kwa wanamichezo waliofanya

vizuri kwa mwaka 2018. Hafla hiyo itafanyika kwenye mji wa Dakar, Senegal.

Wanamichezo mbalimbali watazawadiwa akiwemo Pierre-Emerick Aubameyang, Sadio Mane na Mohamed Salah wameingia katika tatu bora kuwania tuzo hiyo. Pia Tuzo zitatolewa kwa wanawake na wanasoka wa kada mbalimbali.

JANUARI 9

Kamati ya Itendaji ya CAF itakutana mjini Dakar kuamua nani atakuwa mwenyeji wa fainali za Afrika mwaka huu kati ya Misri na Afrika Kusini ambazo zinachukua nafasi ya Cameroon ambayo imenyang’anywa uwenyeji kwa kushindwa kujipanga.

Misri iliwahi kuandaa fainali za 2006 wakati Afrika Kusini ilichukua nafasi ya Libya 2013 kutokana na machafuko yaliyotokea nchini humo.

JANUARI 11

Kuanza kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni baada ya miamba ya Tunisia, Esperance na Al Ahly ya Misri kufanya vizuri fainali zilizopita.

Timu 16 zinaingia kwenye kinyang’anyiro hicho zikiwemo 10 za zamani na baadhi ya timu mpya kwenye michuano hiyo ikiwemo CS Constantine, JS Saoura ya Algeria na mabingwa wa Zimbabwe, FC Platinum. Mechi za makundi zitaendelea hadi katikati ya machi zitakapoingia robo fainali.

JANUARI 22

Droo ya mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya mechi za mchujo zinazoanza Januari 13 hadi 20.

Timu zitakazofuzu zitatengeneza idadi ya timu 16 zitakazogawanywa katika makundi manne.

FEBRUARI 2

Nigeria itakwenda Niger kuwania taji la nane la Fainali za Afrika kwa vijana wa U-20 na washindi watakwenda kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Poland baadaye Mei.

Timu nane zitakuwa kwenye miji ya Maradi na Niamey, ambazo ni Burkina Faso, Burundi, Ghana, Mali, Senegal na Afrika Kusini.

FEBRUARI

Hadi sasa haijafahamika ni lini itachezwa mechi ya Super Cup kati ya Esperance ya Tunisia na Raja Casablanca na mpango ilikuwa ikachezwe Qatar hatua ambayo imepigwa vikali kupelekwa huko lakini hata hivyo, bado tarehe ya mechi hiyo haijapangwa.

MACHI 19-21

Tarehe ya mechi za mwisho kwa mechi za kuwania kucheza Fainali za Afrika 2019 timu zikiwania nafasi 10 zilizosalia kupata wawakilishi.

Mataifa yanayotajwa kuwa na nafasi ya moja kwa moja ni Burundi, Visiwa vya Comoro na Lesotho ambazo zitaungana na wageni waliokwishafuzu ambao ni Madagascar na Mauritania. Hapa ndipo hukumu ya Taifa Stars itatoka dhidi ya Uganda na kuangalia mwelekeo wa Lesotho na Cape Verde. Bado siku 105.

APRILI 14

Kuanza kwa fainali za Afrika kwa Vijana wa U-17 ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji wake. Mechi hizo zitachezwa kwa wiki mbili na timu nne za kwanza zitakwenda Peru kwenye Fainali za Kombe la Dunia za U-17.

Timu zitakazoshiriki ni Angola, Cameroon, Guinea, Morocco, Nigeria, Senegal na Uganda.

Miamba hiyo ilipatikana katika michuano iliyochezwa kwa ngazi ya kanda kwa mara ya kwanza.

MEI 26

Tarehe ya kumalizika kwa mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

MEI 31

CAF imepanga mechi ya pili ya fainali ya Ligi ya mabingwa kuchezwa.

Itakuwa mwisho wa mashindano ya Afrika ngazi ya klabu ikikamilisha miezi sita ya mchakamchaka wa mashindano ya CAF ambayo ni mara ya kwanza kumalizika Mei ikianza na mwaka huu.

CAF imelazimika kubadili tarehe za kuanza na kumalizika mashindano yake kwa kuwa ligi za mataifa mengi zinaanza Agosti na kumalizika Mei ya mwaka unaofuata.

JUNI 5

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino atapokea taarifa za mapendekezo ya uchaguzi wa Rais wa Fifa kwenye Mkutano Mkuu wa Fifa utakaofanyika Paris, Ufaransa.

Hata hivyo, mpaka sasa hakuna mgombea aliyejitokeza kusema anataka nafasi hiyo na Infantino anaweza asipate mpinzani akaendelea kuula miaka mingine minne ijayo.

JUNI 7

Afrika Kusini itacheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa huku Nigeria ikizikosa fainali hizo.

Cameroon inaingia kwa mara ya pili ikipangwa na Canada, Uholanzi na New Zealand. Banyana Banyana itaanza na Hispania Juni 8.

JUNI 15

Kuanza kwa Fainali za Afrika safari hii zikishirikisha timu 24 kwa mara ya kwanza japokuwa mwenyeji bado hajafahamika.

Timu zitagawanywa kwenye makundi sita ya timu nne na timu 16 zitaingia hatua ya mtoano.

Timu nne kati ya sita itakayoshika nafasi ya tatu katika zitakata tiketi baada ya mechi tatu. Fainali itachezwa Julai 13.

JULAI

Hakuna tarehe hasa iliyopangwa kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika nchini Qatar. Afrika itakuwa na timu tano katika fainali hizo za mwisho kwa timu 32 na zitakazofuata zitakuwa na timu 48.

AGOSTI 16-18

Tarehe ambayo kutachezwa mechi ya ufunguzi ya michuano ya klabu Afrika ya 2018-19 ya Super Cup ambayo ni kwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa na Bingwa wa Kombe la Shirikisho.

AGOSTI 9

Kuanza Michuano ya Klabu Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Mechi zake zitamalizika Mei 2020. Michuano ya mwaka huu inatimiza miaka 56 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.

OKTOBA 9

Siku ya kupanga droo ya ligi ya mabingwa na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho ambayo shughuli nzima inafanyika Makao Makuu, Cairo.

OKTOBA 11

Kuanza kwa mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 Kanda ya Afrika na zile za Afrika 2021 lakini CAF haijapanga tarehe.

CAF ilikutana Moscow wakati wa Fainali za Kombe la Dunia na walikubaliana kwamba mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia na zile za Afcon 2021 zitachezwa tofauti.

Kulikuwa na mapendekezo kuwa timu zitakazofuzu Afcon ndizo ziwe zimefuzu Kombe la Dunia lakini hoja hiyo ikakataliwa.

NOVEMBA 19

Fainali za Afrika za U-23 zitafanyika Misri na timu zitakazoshika nafasi tatu za juu zitashiriki Michezo ya Olimpiki ya 2020 Japan.

NOVEMBA 29

Kuanza kwa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2019-20.

DESEMBA 11

Tarehe ya kuanza mechi za Fifa ngazi ya klabu na safari hii zitafanyika China. Afrika haijawahi kufanya vizuri Fainali za Klabu, mara ya mwisho ilikuwa 2013 kwa Raja Casablanca kushika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Bayern Munich katika fainali.

Advertisement