Ndani ya boksi: Stamina amegonga A+ darasa la kina Lady Jaydee na Sir Nature

Lile dude “Asiwaze” ambalo Stamina ameliungurumisha ni noma. Nilipoisikia ngoma yenyewe, nikasema ewaaah, Mluguru Stamina tayari ameshabukua A+ tena ya pointi 7 katika darasa la Lady Jaydee, Juma Nature, Diamond Platnumz na wengine.

Unalijua darasa la Lady Jaydee? Ni hivi mwanafunzi wa darasa hilo akifaulu vizuri, kaa naye mbali. Akiwa mpenzi wako, siku mkimwagana utajikuta kwenye nyimbo. Hilo darasa walimu wakuu ni Jaydee na Juma Nature. Mtafute Sinta akwambie shombo za Nature, walipotibuana na kumwagana. Nature alijaza albamu akilishughulikia hilo.

Tuanze na Lady Jaydee

Huyu ni Malkia wa Afro-pop wa wakati wote nchini. Yeye anao msururu wa nyimbo ambazo kwa tafsiri za wengi ni kuwa alimuimba aliyekuwa mume wake.

Ukiachana na nyimbo za nyuma kama ‘Wanaume Kama Mabinti’, ‘Usiusemee Moyo’, ‘Siri Yangu’ na nyingine, kuelekea kuvuja kwa siri kuwa Jaydee na aliyekuwa mumewe wameachana, alitoa wimbo ‘Nasimama’ ambao ulionekana moja kwa moja kugusa ndoa yake.

Ndani ya wimbo huo, lipo gazeti la kila wiki lililoandika habari kwa herufi kubwa “Jaydee Aomba Talaka”, akaoanisha na tukio la kutendwa na mume wake kwa kumfanyia usaliti. Watu wa karibu yake wakasema aliimba na kurekodi video kwa mujibu wa tukio halisi.

Baadaye ikavuja kuwa tayari wameachana kisha wote wakakiri. Moja ya sababu ambazo Jaydee alieleza ya kuachana kwao ni kuwa mumewe hakuwa mwaminifu. Video ya Nasimama ilishaonyesha kabla.

Wimbo ‘Yahy’a kuna mtu mjanjamjanja wa mjini (jina lipo), alikiri kutibuana na Jaydee ndipo akakutana na mashairi makali. Wimbo mpya ‘Ndi Ndi Ndi’ pia ulitoa mwelekeo wa aina hiyo, ingawa mwenyewe alikanusha.

Ndani ya ‘Ndi Ndi Ndi’ Jaydee anaimba kuwa huyo mtu alimpeleka Hospitali ya Mirembe na geti limeshafungwa. Ukitaka umaarufu mchokoze Jaydee. Utaona matokeo yake atakapoingia studio na kukutolea wimbo wa kukunanga. Mwite Binti Komando, Mama Samefood, Binti Machozi kisha malizia Mama Ndi Ndi Ndi.

Katika ‘Asiwaze’, Stamina ameonyesha kuwa darasa la Lady Jaydee alilielewa. Kwamba ya nini uzinguliwe kimanzi halafu ukae kimya wakati topik umeshapata? Ni suala la kuingia ‘booth’ halafu kinawaka. Stamina amekiwasha ile kinoma.

Juma Nature aliua

Mwigizaji Sinta hana hamu naye hata kidogo. Albamu ya ‘Ugali’ iliyotoka mwaka 2003, ilikuwa na nyimbo tatu zenye mashambulizi kwa mrembo huyo ambaye alipata kuwa mpenzi wake kabla ya kuachana.

Nyimbo mbili, ‘Sitaki Demu’ nakala mbili (original na remix), zilimgonga moja kwa moja lakini funga kazi ilikuwa ‘Inaniuma Sana’ ambayo ndani yake Mfalme wa Temeke (Nature) alilalamika mpaka kujiliza.

Hata wale ambao walikuwa hawamfahamu Sinta (japo alikuwa maarufu mno kipindi hicho), ilibidi wamfuatilie na kumfahamu.

Huyo ndiye Juma Kassim Kiroboto, alipokorofishana na aliyekuwa meneja wake, Said Fella, ugomvi wao aliusindikiza na wimbo ‘Ndege Tunduni’, ndani yake mashairi yakiimba “Mshike mshike Ndege Tunduni, sisi wajanja tumekimbia, mshikemshike Ndege Tunduni, waliobaki wataumia.”

Bila shaka baada ya Nature kusikiliza Asiwaze, atakuwa amefurahi sana. Maana ametii falsafa yake ya “nitibue kimapenzi nikujazie nzi kwa kukuimba kila mtu ajue na akujue”. Aisee baada ya mashambulizi ya Nature na Sinta ndio ikawa bye. Alipotea.

Hata Diamond

Jina kamili ni Nasibu Abdul Juma, mwenyewe kutokana na mafanikio yake, siku hizi anajiita Dangote ‘Chibu Dangote’, akijifananisha na mfanyabiashara mkubwa anayetajwa kuwa tajiri namba moja Afrika, Alhaj Aliko Dangote.

Ni mkali wa kuandika na kuimba matukio yake. Mwenyewe katika mahojiano kadhaa amepata kukiri kuwaimba wanawake wake wa zamani kwenye nyimbo zake.

Diamond hulalamika mno kwenye nyimbo mithili ya mtu anayeonewa katika mapenzi, ingawa wakati mwingine huonyesha majuto yake. Isisahaulike wimbo ‘Number One’ nakala ya kwanza ina kibwagizo “na mtuache tulale” litakuwa dongo kwa aliyekusudiwa.

Vivyo hivyo alifanya katika wimbo ‘Utanipenda’ alifikisha ujumbe kwa jamii, lakini kwa mwandani wake pia.

Diamond bwana! Akatoa “Sikomi” humo amejiliza kwa matukio ya kweli na wapenzi wake. Hivi karibuni alitoa mzigo “Baba Lao” humo ndani ni tambo na majigambo. Eti hata wakiungana hawamuwezi.

Watu na silaha zao za kinywa kwa kusindikiza midundo ya muziki, wachokoze Emmanuel Elibariki ‘Nay Wamitego’, Ibrahim Mussa Mshana ‘Roma Mkatoliki’, Haruna Kahena ‘Inspector Haroun’, Hamad Ally ‘Madee’, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ uone.