Breaking News

AT: Msanii aliyesomesha ndugu zake wanne kwa muziki

Saturday October 12 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Unapowataja wasanii wa muziki wa kizazi kipya waliofanya vizuri kwenye miondoko ya mduara huwezi kuacha kumtaja, Ally Ramadhani maarufu kama AT.

AT pamoja na vibao vingine alivyoachia kama ‘Nipigie’ alichomshirikisha Stara Thomas, ‘Mama ntilie’ alichoimba na Ray C na Gelly, ‘Bado’ ‘Vifuu Tundu’ na ‘Bao la Kete’ ni nyimbo zisizoisha hamu kuzisikiliza licha ya kuchezwa miaka kadhaa iliyopita.

Mahadhi yake yaliyonogeshwa na upigaji wa vyombo vya asili unazifanya nyimbo hizi kila zinapopigwa kwenye shughuli mbalimbali watu kujikuta wakiinuka kwenye viti vyao na kwenda kucheza.

Gazeti hili lilifanya mahojiano na staa huyo kujua pamoja na mambo mengine sababu za kupotea kwenye muziki licha ya kufanya vizuri.

Swali: Ilikuwaje ukajikuta unaingia kwenye muziki

Jibu: Nilikua napenda kusikiliza pia home, wazee wanapenda muziki babu yangu mzaa baba alikua mshairi.

Advertisement

Hata hivyo niliingia rasmi katika muziki mwaka 2003 niliposhiriki mashindano ya kuimba yaliyoandaliwa na mmiliki wa studio ya Chuchu na kuibuka mshindi kati ya jumla ya washiriki 120.

Hawa ndio walikuwa watu wa kwanza kuniingiza studio, na kupika kibao cha ‘Msile Ndimu’ kilichofanya vizuri Zanzibar.

Swali: Tangu mwaka 2010 na 2011 ulipotamba na vibao vya ‘Vifuu Tundu ‘ na ‘Bao la Kete’. ulipotea umepotea sana nini tatizo?

Jibu: Hakuna tatizo nilihisi muda wangu umepita waje wengine nami nijipange upya.

Swali: Unadhani kuadimika kwako kuna aliyekupoteza kwenye muziki wa mduara?

Jibu: Hapana maana mpaka leo hakuna aliyechukua nafasi yangu, mashabiki wa muziki wangu wapo wananisubiri nami nipo tayari watarajie kupata ladha kutoka kwangu hivi karibuni.

Swali: Mbali ya mduara unaweza kuimba muziki wa aina gani?

Jibu: Mimi naweza kuimba muziki wowote ule, aina ya muziki ninaoimba unanifanya niwe na uwezo wa kuimba miondoko yote. Angalia nimefanya aina hiyo hakuna mtu aliyefuata nyayo zangu, ninaimba katika njia ngumu za Kiajemi, hakuna msanii wa Bongofleva anayeweza.

Swali: Je, nyimbo za ‘Vifuu Tundu’ na ‘Bao la Kete’ zilikuletea mafanikio gani katika maisha yako ambayo hutakaa ukasahau

Jibu: Nilifanyia mambo mengi ila zaidi kusomesha wadogo zangu wanane ambapo kidogo nilijona mimi ni mwenye uwezo na hata gari ambalo ninalimiliki lilikuja kama zawadi tu.

Pia mpaka leo bado nahisi nina deni kubwa kwa wazazi wangu ndio maana naendelea kupambana kuwafanyia jambo kubwa kwani kipindi kile fedha za muziki tulizokuwa tunapata huwezi kulinganisha na wanaozipata wanamuziki wa sasa.

Swali: Kama usingekuwa msanii, ungekuwa nani

Jibu: Ningelikua fundi kuchomelea kwani nilisomea kazi hii na nilishawahi kuifanya.

Mbali na kuchomelea nishasomea masuala ya ushauri nasaha kwa waathirika wa dawa za kulevya na Ukimwi.

Kama haitoshi nilishafanya kazi katika kiwanda cha kuoka mikate na kuuza samaki kwa miaka mitatu, kazi niliyoianza nikiwa nasoma darasa la saba na kuacha nikiwa kidato cha pili, yote ni kutokana na familia yangu kutokuwa na uwezo.

Swali: Uliwezaje kufanya kazi huku unasoma

Jibu: Nilikuwa nikitoka shule jioni naenda kuuza samaki gengeni hadi usiku

Swali: Kati ya wasanii watatu ambao leo ungeambiwa uwachague kufanya nao kazi ni nani na kwa nini?

Jibu: Sabaha Salum, Pauline Zongo na Juma Kakere kwa kuwa naona kuna shani ndani yao na mimi huwa siangalii jina bali naangalia ubora wa kazi.

Mfano wakati wa kibao cha ‘Nipigie’ walikuwepo wengi wanafanya vizuri ila niliona shani kwa Stara Thomas.

Advertisement