Aneth kielelezo kuwa masomo ya sayansi si magumu

Tuesday April 9 2019

 

Imekuwa ikiaminika kuwa watoto wa kike wengi wanaogopa masomo ya sayansi na kukimbilia kuchagua masomo ya biashara au sanaa kwa kuwa ndiyo rahisi kuyasoma na hata baadaye kutoka kimaisha.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba kuna wanawake wamefanya mengi katika ugunduzi wa vitu mbalimbali duniani baada ya kusoma vema na kuipenda sayansi. Wao na sayansi, sayansi na wao tangu wakiwa wadogo na wanafanya vizuri hadi sasa kuliko hata wanaume.

Miongoni mwao ni binti wa Kitanzania, Aneth David (29), Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi Shahada ya Uzamivu (PhD) aliyejikita kufanya utafiti wa namna viumbe vidogo vidogo vilivyo kwenye udongo (soil microorganisms) vinavyoweza kuongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo nchini.

Utafiti wake unajaribu kuelewa uhusiano kati ya viumbe hivyo na mfumo wa kilimo wa sukuma-vuta. Mfumo huu unatumiwa na wakulima wa mashariki na kusini mwa Afrika kupambana na visumbufu vya ‘stem borers’ na magugu aina ya kiduha ambayo husumbua mazao ya nafaka hasa mahindi na mtama.

“Matokeo ya utafiti huu yanaweza kutumiwa kuboresha mfumo wa sukuma-vuta kuupa tija zaidi na kuongeza uzalishaji wa mazao husika,” anasema Aneth.

Kwa mfumo wa elimu nchini na umri wake huenda ukapata maswali mengi likiwemo kama alisoma nje kutokana na mafanikio yake ya haraka ya kitaaluma.

Imekuwaje binti wa miaka 29 akafika ngazi hiyo kubwa ya kitaaluma hususan katika masuala ya sayansi ambayo yametawaliwa na wanaume tu?

“Nimesoma elimu yangu ya msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro na shahada yangu ya kwanza na umahiri nimesomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” Aneth ameiambia Nukta katika mahojiano hivi karibuni.

Binti huyo alisoma Shule ya Sekondari ya Mawenzi kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na Shule ya Sekondari ya Majengo katika elimu ya kidato cha tano hadi sita.

Ile dhana ya kuwa tatizo ni ubora hafifu wa shule nchini ndiyo sababu ya wasichana hawasomi sayansi kwake haifanyi kazi. Sayansi kwake ni wito wa ndani wa mtu unaoweza kumpeleka mbali kama akiamua kuamini katika ndoto zake

Licha ya kuwa hasikiki kama walivyo baadhi ya wanawake nchini, Aneth amewahi kupata tuzo ya balozi wa sayansi ambayo hutolewa na Jukwaa la Next Einsteins Forum (NEF).

Jukwaa hilo linakuwakutanisha Wanasayansi na wadau mbalimbali duniani ili kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili Afrika na maeneo mengine ulimwenguni.

Ushindi huo ulimfungulia milango mingi zaidi ndani na kumpa uwanja mpana wa kuchangia katika kuleta mabadiliko kwenye sayansi na teknolojia Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Sio lazima wote tuwe wahandisi au wahadhiri au watafiti, wanasayansi wanahitajika kwenye kila eneo kwa sasa nchini na duniani kote,” anasema Aneth.

Anawazaje kumudu vyote hivyo kwa pamoja?

Hata hivyo, kutokana na umri wake na vitu anavyofanya Aneth amesema kuwa kitu kikubwa anachofanya ni kupanga ratiba yake ili usiingiliane na muda wa kufanya utafiti ambao ameanza tangu mwaka 2016.

“Najipangia malengo ya kila wiki, mwezi, robo mwaka na mwaka, supervisors (wasimamizi) wangu wa PhD wanasaidia sana kuhakikisha ratiba ya shule inaenda na muda wangu haumezwi na mambo mengine ya nje.” Kwenye masomo ya sayansi, kwa mujibu wa Aneth, kuna fursa nyingi na maeneo mengi ya kushiriki ambayo kila mtu anaweza kupata nafasi kama kwenye mambo ya tiba, lishe, viwanda ,Tehama na mengineyo ni swala la kuchagua nini kinakufaa na kukifanyia kazi.

Ujumbe wake kwa watoto wa kike waliopo mashuleni ni kuwa watafute mifano hai ya wanasayansi wanawake ili wapate kuwa chachu kwa maendeleo yao na kujifunza kutoka kwao

Advertisement