Askofu Ruwa’ichi ana mamlaka makubwa kuliko Kardinali Pengo

Muktasari:

Siku 34 baadaye, yaani Machi 25, 2018, Polycarp Kardinali Pengo, askofu mkuu wa Dar es Salaam, aliupinga.

Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) lilipotoa ujumbe wa Kwaresima 2018, Askofu Mkuu Jude Thadaeus Ruwa’ichi wa Mwanza ndiye aliyeutetea Radio Vatican.

Siku 34 baadaye, yaani Machi 25, 2018, Polycarp Kardinali Pengo, askofu mkuu wa Dar es Salaam, aliupinga.

Hili si jambo la ajabu. Hata mwaka 1968, kitabu cha Padre Joseph Ratzinger (baadaye Papa Benedicto wa 16) cha Introduction to Christianity, kiliwagonganisha maaskofu wa Poland.

Jijini Warsaw, Stefan Kardinali Wyszyński alikipiga marufuku kitabu hicho. Lakini Józef Kardinali Wojtyla (baadaye Papa John Paul II) alikipenda, akakiruhusu jimboni mwake Krakówm, kwa mujibu wa kitabu cha wasifu wa Ratzinger.

Pamoja na kukizuia kitabu hicho nchini Poland, kumpinga Kardinali Wyszyński ilihitaji ujasiri kwa kuwa wengi walidhani ndiye mkuu wa Kanisa Katoliki nchini humo.

Na hii ni kutokana na vyeo au madaraka ya viongozi wa kanisa hilo kuwachanganya wengi kama ilivyo kwa askofu mkuu (arch Bishop) na askofu mkuu mwandamizi (Co-adjutor Bishop) na hasa sababu zake.

Maaskofu waandamizi Tanzania

Alipoteuliwa Jude Thadaeus Ruwa’ichi kuwa “askofu mwandamizi” mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam ilizungumzwa sana, wengi wakihoji mamlaka ya Kardinali Pengo. Hata kabla ya mjadala huo, kwanza tuone kuwa haya si madaraka mapya nchini au duniani.

Ruwaichi ni askofu mwandamizi wa saba nchini. Wa kwanza ni Joseph Sweens, askofu mwandamizi wa Mwanza aliyeteuliwa Januari 01, 1910 akarithi kanisa Desemba 12, 1912.

Wa pili alikuwa Henri Léonard, askofu mwandamizi wa Tabora, aliyeteuliwa Juni 26, 1912 akarithi kanisa kesho yake tu. Akafuata Victor Haelg, askofu mwandamizi wa Lindi, aliyeteuliwa Januari 13, 1949 akarithi kanisa Desemba 15, 1949.

Novemba 14, 1988 Tarcisius Ngalalekumtwa aliteuliwa kuwa askofu mwandamizi wa Jimbo la Sumbawanga.

Vilevile, Polycarp Pengo aliteuliwa Januari 22, 1990 kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Dar Salaam na akarithi jimbo Julai 22, 1992.

Castor Msemwa “askofu mwandamizi” wa Tunduru-Masasi aliteuliwa Desemba 07, 2004 akarithi jimbo Agosti 25, 2005. sababu kubwa ya wote hao kuteuliwa ni kuwapo kizuizi cha majukumu.

Kizuizi cha majukumu

Kifungu cha 1121 cha Katekismo ya Kanisa Katoliki kinasema Mkatoliki akishapata ubatizo, kipaimara, ushemasi, upadri au uaskofu inakuwa moja kwa moja, havifutiki na ni majukumu ya kudumu. Hivyo, mtu hawezi kustaafu majukumu hayo ya kudumu. Kifo tu ndicho humstaafisha.

Desemba 20, 1623, Askofu Pedro Quinones wa Seville, Hispania, alifia madarakani akiwa na umri wa miaka 90. Mwaka 678, Papa Agatho aliteuliwa akiwa na miaka 101 akafia madarakani akiwa na miaka 104, ikimaanisha kuwa hakuna kilichozuia majukumu yao isipokuwa kifo.

Hivyo, kizuizi tu ndicho husitisha jukumu la mkatoliki. Vizuizi kikimtikisa “askofu wa jimbo” kinaitwa “sede impedita”. Vizuizi vikuu vya askofu, Mbali na kifo, ni kutishwa na serikali na kuchoka au kuugua. Mengine ni mtu kujitakia pale anapogeuka kero.

Mfano, Mei 1987, Thomas Donnellan, askofu wa Atlanta, Marekani alipooza (stroke) kwa miezi mitano au mwaka 1809 Papa Pius VII alipotekwa na makachero wa serikali, hivyo ni vizuizi vya kazi za uaskofu na askofu mwandamizi anaweza kuteuliwa.

Umbali kutoka Roma

Roma hupata taarifa za jirani kirahisi na kuzifanyia kazi haraka. Hivyo, tangu zamani kizuizi kilipomtinga askofu wa karibu, alijiuzulu au aliondolewa mapema.

Lakini kizuizi kilipomkumba askofu wa mbali, enzi hizo usafiri ukiwa wa farasi au jahazi, moja ya mbinu ilikuwa ni kupeleka “askofu mwandamizi”, yaani “co-adjutor bishop” kama alivyo Yuda Ruwa’ichi.

Mfano, Julai 01, 1505, askofu Jean Grimaldi wa jimbo la Grasse (France) alifariki dunia, askofu mwandamizi Agostino Grimaldi akarithi jimbo na mifano kama hiyo mingi. Hii ndiyo historia ya kuwapo “askofu mwandamizi”, kigezo kikiwa kuondoa kizuizi “sede impedita”.

Kuishiwa uwezo

Askofu Jude Thadaeus Ruwa’ichi alipopokewa jimboni Dar es Salaam Septemba 07, 2018, Kardinali Pengo alisema, “anayeomba msaada kama huu wa kwangu, maana yake anaonekana kuchoka.” Wengine hutumia neno “incapacitatem”

Gazeti la ofisi ya Papa, L’Osservatore Romano, Machi 06, 2013 ni lilichambua neno “incapacitatem” alilotumia Papa Benedict XVI kwenye barua yake ya kujiuzulu upapa kuwa ni “kizuizi cha kuchoka” kinacholeta “sede impedita” na kinaweza kumleta “askofu mwandamizi”.

Papa Benedict XVI alitumia kilatini “incapacitatem” wakati Kardinali Pengo kwa Kiswahili alitamka “kuchoka” lakini maana ni ileile.

Umri wa kustaafu

Wapo wanaodhani kwamba “askofu wa jimbo” akikaribia umri wa miaka 75 analetewa “askofu mwandamizi”. Hii si kweli.

Novemba 02, 1995 jimboni Palmerston North, New Zealand, askofu James Cullinane mwenye umri mdogo wa miaka 59 alipelekewa “askofu mwandamizi”, John Dolan, mwenye umri mkubwa wa miaka 67.

Vilevile, Aprili 22, 2010 jimboni “Ha Noi”, Vietnam, Askofu Joseph Kiet akiwa na miaka 58 alipelekewa “askofu mwandamizi”, Pierre Nhon, mwenye umri mkubwa wa miaka 72.

Hivyo, umri si kigezo cha kuleta “askofu mwandamizi”.

Sheria ya John Paul II

Hata hivyo, Januari 24, 2004, Papa John Paul II aliidhinisha sheria iwaongoze maaskofu.

Kanuni ya 72 ya sheria hii (Apostolorum Successores), sentensi ya kwanza inasema, “Pale hali inapolazimu Papa anaweza kuteua “askofu mwandamizi”.

Udadisi wa waandishi

Mipango ya kumdhibiti John Kardinali Cody, askofu wa jimbo la Chicago, ilitafitiwa na John Conroy wa gazeti Chicago Reader la Juni 04, 1987 na kitabu cha David Yallop – In God’s Name.

Waandishi hao wote wanasema Papa John Paul I asingefariki ghafla Septemba 28, 1978 uteuzi wa askofu mwandamizi ungeyazuia madaraka ya Kardinali Cody.

Madaraka ya mwandamizi

Je, ni kweli askofu mwandamizi ni mdhibiti wa askofu wa jimbo? Sentensi ya tatu ya kanuni ya 72 ya sheria Apostolorum Successores inamzuia “askofu wa jimbo” kufanya mambo yasiyoruhusiwa na “askofu mwandamizi”.

Hata Papa John Paul II asingetunga sheria hii, tumeona askofu mwandamizi huletwa iwapo kizuizi kimeshamtinga au kimemkaribia kumtinga askofu wa jimbo.

Wengine husema kizuizi ni kushindwa kuhubiri hata kwa barua. Sivyo. Aprili 18, 2017, Papa Benedict XVI alipotimiza miaka 90 alifurahia keki na bia za kijerumani, akahubiri mbele ya Waziri Mkuu wa Bavaria.

Baraza la maaskofu

Rais wa Baraza la Maaskofu ni mtu mwenye waumini jimboni. Mwaka 2006, Rais wa Baraza la maaskofu Kenya alikuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Nyeri, John Njue. Hata wa Vietnam, Aprili 22, 2010 alikuwa ni yule askofu mwandamizi, Pierre Nhon.

Hivyo, Jude Thadaeus anaweza kuwa rais wa “TEC”, lakini Method Kilaini, Eusebius Nzigilwa au Balthazar Lyimo hawawezi, wao ni “titular bishops”, hawana waumini.

David Yallop anasema waumini ni wa askofu mwandamizi na askofu wa jimbo hubaki kama “titular bishop”. Ninamnukuu, (Iliafikiwa kuwa Cody aelezwe kuwa ni lazima akubali askofu mwandamizi wa kuendesha shughuli zote za Jimbo. Yeye angeruhusiwa kukaa tu na cheo bila mamlaka ya Chicago).

Utii kwa “askofu mwandamizi”

Je, mapadri, masista, waumini wamtii nani sehemu yenye “askofu mwandamizi?” Kwanza naamini “sede impedita” imeeleweka. Pili, mapadri waliapa kutii “waandamizi” tangu siku ya upadrisho.

Tatu, tumeona kanuni ya 72 ya “Apostolorum Successores” inavyomgeuza “askofu wa jimbo” kuwa mtiifu wa anayoyataka “askofu mwandamizi”.

Nne, barua ya Papa Francis kwa Jude Thadaeus imeagiza kila mtu kuwa mtiifu kwa Askofu Jude Thadaeus.

“Tunakuagiza kuwajulisha barua hii wakheri na watu wote wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Hao wote ni wana wapenzi tunawahimiza, wakupokee na kukuheshimu, wakiungana nawe katika umoja.”

Kumsimika askofu mwandamizi

“Misa ya mapokezi” ya Jose Gomez, askofu mkuu mwandamizi wa Los Angeles, ilifanyika Mei 26, 2010.

Askofu wa jimbo hilo, Roger Kardinali Mahony alisema, askofu mwandamizi akishawasili kiti cha askofu (kathedra) hakiwezi kuwa wazi.

Kardinali Mahony akasema tahadhari nzuri ni kumkalisha kabisa “askofu mwandamizi” kitini siku anapowasili.

Kardinali Mahonyi alipomaliza kusema hayo, akamkalisha “askofu mwandamizi” kwenye “kathedra” ndipo akamalizia ile misa ya mapokezi.

Kumketisha askofu kwenye “kathedra” ni “kusimikwa”. Hivyo, siku ya kumpokea “askofu mwandamizi” baadhi wameanza kuiita ni siku ya “kumsimika”.

Rekodi za David Talley zinasema Novemba 07, 2016 “alisimkwa” kuwa “askofu mwandamizi” wa Alexandria, Marekani, akarithi jimbo hilo Februari 2, 2017.

Matatizo ya uaskofu mwandamizi

Uaskofu mwandamizi pia una matatizo, mzoefu nchini ni Tarcisius Ngalalekumtwa aliyeutumikia kwa miaka minne bila kurithi jimbo.

Laurean Kardinali Rugambwa alipofariki askofu Pengo alinukuliwa akisema: “Uvumi kwamba nimekataa kumzika Dar es Salaam si kweli, kama niliweza kuishi naye akiwa hai, ningeshindwaje kuishi naye akiwa kaburini?” (Tanzania Daima Oktoba 07, 2012).

Kardinali Cody alipohisi Joseph Bernadin angeletwa awe “askofu mwandamizi” Chicago, alinuia kumkomoa hata kwa kusaidiwa na makachero serikalini, yaani FBI, kwa mujibu wa Chicago Reader.

Makachero wa Poland walimuwinda na kumpekua sana Kardinali Wojtyla. Hivyo, Kardinali Wojtyla alipoteuliwa kuwa Papa John Paul II, alisubiri hadi kifo cha Kardinali Cody, ndipo akampeleka Joseph Bernadin bila bugudha za makachero.

Kardinali Wojtyla, angekuwa askofu mwandamizi wa Warsaw basi Kardinali Wyszyński asingezuia kitabu cha Joseph Ratzinger aliye Benedict XVI wa sasa.

Kwa mtririko huio endapo Pasaka 2018 ingemkuta Jude Ruwa’ichi akiwa askofu mwandamizi Dar basi, “askofu wa jimbo” asingeupinga waraka wa Kwaresima.

Hii ni kutokana na kanuni ya 72 ya “Apostolorum Successores” ambayo ingemzuia askofu wa jimbo kupinga waraka bila ruhusa ya askofu mwandamizi anayeupenda waraka.

Mgongono wa nafasi hizo uko dunia nzima. Mwaka 1870 maaskofu mkutanoni (Vatican I) walipendekeza bila mafanikio, uaskofu mwandamizi ufutwe iwe rahisi kuishi na askofu msaidizi yaani auxiliary bishop kuliko mwandamizi.

Tatizo askofu msaidizi ni chaguo la askofu wa jimbo, hivyo ombi lilipokataliwa tuliepusha uwezekano wa askofu kupandikiza mtu wake kurithi jimbo.

Mwisho ni maoni yangu kuhusu matumizi sahihi ya lugha, kwamba “askofu mwandamizi” si neno sahihi, usahihi kumaanisha Co-adjutor Bishop, huyu ni “askofu mwenza”. Hata “co-wife” hatumwiti “mke mwandamizi,” tunamwita “mke mwenza”.

Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa Mwananchi na mchambuzi wa masuala ya Kanisa Katoliki anayepatikana kwa simu 0754-710684, email: [email protected]